MSAJILI wa Hazina, Dk. Oswald Mashindano, amesema benki na taasisi za fedha haziruhusiwi kuendelea kutoa mikopo kwa kiwanda chochote kinachotumia hati za serikali kama dhamana bila ruhusa ya ofisi yake.
Amesema ofisi yake imefikia uamuzi huo baada ya kubaini tabia ya baadhi ya wamiliki wa viwanda waliopewa dhamana na serikali kuvisimamia, ambao hukiuka mikataba kwa kujipatia fedha, ambazo hawazitumii kwenye kuendeleza viwanda husika.
Msajili amesema pamoja na hatua hiyo, anawaonya wawekezaji wanaotumia ujanja kuiba mali za serikali kwa hila, ikiwemo kubadili nyaraka muhimu kwamba, serikali inawafuatilia na haiko tayari kupoteza kitu kwa sasa.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, jana, Dk. Mashindano alisema hatua zinazochukuliwa na ofisi yake kwa wakati huu ni kupitia upya mikataba ya ubinafsishaji kwenye viwanda na mashamba yote ili kujiridhisha juu ya uhalali wake.
"Kuna timu ya watu wetu inazunguka nchi nzima kuangalia viwanda hivi, kuainisha na kupitia mikataba iliyotumika na hivi tunavyozungumza iko Shinyanga, kwa sababu tunakubali kwamba, kama ilivyokuwa kwenye madini, baadhi ya mikataba yetu ina matatizo kisheria.
"Baadhi ya mikataba ina vipengele vinavyoruhusu serikali kuzungukwa kwenye usimamizi wa kiwanda, mingi haina vipengele vinavyoipa nguvu serikali kuchukua kilicho chake pale mwekezaji anaposhindwa kutimiza makubaliano, hasa ya kuzalisha maradufu," alisema.
Dk. Mashindano aliongeza kuwa, matatizo ya kisheria kwenye mikataba ya aina tatu inayotumiwa na serikali kwenye ubinafsishaji wa viwanda, ikiwemo mufilisi, mauzo ya mali na uuzaji wa hisa, yalisababishwa na kukosekana kwa uzalendo kwa baadhi ya watendaji walioaminiwa na serikali.
Mbali na hilo, aligusia suala la mali za iliyokuwa National Milling, ambayo katika miaka ya hivi karibuni, ilizaliwa kwa sura ya Bodi ya Nafaka kwamba, kuna baadhi ya taasisi za serikali na watu binafsi wamejimilikisha, kupangisha watu wengine na kuchukua kodi, hivyo zinapaswa kurudi.
Alisema National Milling ilikufa kifo cha asili baada ya kutegemea zaidi ruzuku bila ya kuzalisha, hivyo kuilazimu serikali kuiweka pembeni, ambapo mali zake, zikiwemo nyumba za kuishi na majengo mengine zipo chini ya uangalizi wa watu wengine hivyo, ofisi yake imeanza kuzifuatilia.
Kuhusu mwenendo wa Kiwanda cha Urafiki, Dar es Salaam na kile cha Chai, Mponde mkoani Tanga, alifafanua kuwa, viwanda hivyo ni miongoni mwa vilivyopewa kipaumbele na serikali kwenye ufufuaji wake ili vizalishe kwa asilimia zote.
Alisema Kiwanda cha Chai Mponde, ofisi yake ilikamilisha kila kitu na kwamba, hatua iliyobaki ni ndogo, ambayo haiwezi kurudisha nyuma jitihada zilizofikiwa mpaka kufikia sasa, huku kile cha Urafiki akisema wanaendelea na mazungumzo na wawekezaji wa Kichina walioingia ubia na serikali.
Msajili alisisitiza kuwa, ofisi yake na serikali inafanya jitihada zote hizo ili kutetea maslahi ya taifa kwa madhumuni ya kuzinufaisha pande zote mbili kwa usawa, sio kuwatisha au kuwavunja moyo wawekezaji.
Gazeti hili baada ya kupata taarifa hizo, lilifanya uchunguzi mdogo, ambao matokeo yake yalibaini kiwanda cha Mponde, kilichoko wilayani Bumbuli, kimesimamisha uzalishaji baada ya baadhi ya watu kutumia nguvu ya fedha kukwamisha jitihada za serikali za kurudisha ufanisi wake.
Baadhi ya wananchi walipohojiwa na gazeti hili kuhusu kusimama kwa kiwanda hicho, walisema kumerudisha nyuma maisha ya wakazi wa maeneo hayo, ambao shughuli yao kubwa ya kujiongezea kipato ni kupitia utumishi wao kwa kiwanda hicho cha chai.
Mmoja wa kiongozi wa eneo hilo, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kwa hali ilivyo, kiwanda hicho kinashindwa kuendelea kutokana na kuwepo kwa matumizi makubwa ya rushwa ili kuzima nia ya serikali ya awamu ya tano ya kufufua viwanda, kikiwemo cha Mponde.
Kiwanda cha Urafiki kwa upande wake, inasemekana wabia bado hawajatekeleza maagizo ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliyoyatoa mwanzoni mwa mwaka jana, alipozuru kiwandani hapo.
Baadhi ya maagizo yalikuwa ni kuacha kutumia majengo ya kiwanda kama maghala kwa kuondoa bidhaa zingine zisizohusiana na uzalishaji wa nguo zinazohifadhiwa kiwandani hapo na kurudisha mashine zilizouzwa kama chuma chakavu kutoka kiwandani hapo kwa kigezo zilikuwa mbovu ili uzalishaji wenye ufanisi uanze mara moja.
No comments:
Post a Comment