Wednesday 12 July 2017
TRA YAFICHUA MBINU CHAFU, MAPATO YAONGEZEKA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imegunda mbinu chafu zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa lengo la kukwepa kodi.
TRA imebaini kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu walikuwa wakikwepa kodi kwa kutoa risiti kwa wateja zilizopita muda wake na kutoa risiti za mizigo, ambayo inatumika zaidi ya mara mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kwenye ofisi za Makao Makuu ya TRA, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alisema wananchi wanaonunua bidhaa, wanatakiwa kudai risiti, ikiwa ni pamoja na kuikagua kama tarehe ipo sahihi na kiasi kilicholipwa.
"Kuna mtindo umezuka, ambapo wafanyabiashara wanatoa risiti ya juzi au kiwango ulicholipa sicho kinachonekana kwenye siriti. Tumetambua hilo na tunawafuatilia wanaofanya hivyo, wanaoprinti risiti na kuziweka kwenye droo, wakikuona wewe ni king'ang'anizi, wanakupa ya juzi," alisema.
Aliongeza: "Wakati mwingine wanasema risiti ya kusafiria, wanakupa risiti ya kusindikiza mzigo ili ufike, lakini risiti siyo ya kwako. Kwa hiyo mzigo ukifika, wanarudi na hiyo risiti, hivyo inatumika zaidi ya mara mbili."
Kutokana na hali hiyo, alisema TRA itawachukulia hatua kali wale wote watakaogundulika kufanya mchezo huo.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kutoa risiti za EFD, wanapokuwa wanauza bidhaa au huduma huku akitaka wananchi kuhakikisha wanadai risiti wanapofanya manunuzi.
"Hivi sasa kuna zoezi la uhamasishaji na ukaguzi linaloendelea nchi nzima katika sehemu zote za biashara, kukagua wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD pamoja na wananchi wote wasiodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma," alisema.
Mbali na hilo, alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 14.4, kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Kayombo alisema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.67, ikilinganishwa na ya mwaka 2015/16, ambayo yalikuwa sh. trilioni 13.3.
Kuhusu kodi ya majengo, aliwashukuru walipakodi wote kwa muitikio huo na wengine wanaoendelea kujitokeza kulipa kodi hiyo, ambayo mwisho ni Julai 15, mwaka huu.
Alipoulizwa kama wale waliowekewa alama ya X wanatakiwa kulipa kodi, alisema kodi hiyo ya majengo haiwahusu kwa sababu eneo lililopo majengo yao litakuwa na kazi maalumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment