Saturday, 29 July 2017

RAIS MAGUFULI AZIDI KUPONGEZWA


Na Thobias Robert – MAELEZO.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa na Shirika lisilo la kiserikali la ‘We are all needed’ (WAN) kwa agizo lake la kukataza wanafunzi wenye ujauzito kuendelea na masomo katika shule za Serikali.

Pongezi hizo zimetolewa leo Jijijni Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shirika hilo, Bi Salome Lwena alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuunga mkono agizo hilo.

Bi. Lwena amesema kuwa shirika lake liko tayari kumuunga mkono Rais Magufuli katika harakati za kukuza na kuendeleza maadili nchini ikiwemo suala la kupunguza mimba za utotoni.

“Sisi WAN tunaunga mkono kauli ya Mh. Rais kuhusu suala la ukatazaji mimba kwa shule za Serikali za Msingi na Sekondari ili wanafunzi hao wasiathiri wanafunzi wengine kwani wanafunzi wakipata ujauzito wanaathirika kisaikolojia,”alifafanua Mwenyikiti huyo.

Bi. Lwena aliongeza kuwa kauli ya Rais Magufuli imewapa nguvu ya kuzidi kutoa elimu ya kuzuia mimba za utotoni kwa wanafunzi ili wasome hadi watakapokamilisha ndoto zao kwani linajihusisha na shughuli ya kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hapa nchini.

Bi. Lwena  alieleza kuwa, kwa sasa Shirika hilo lina mradi utakaofanyika nchi nzima ujulikanao kama “Protect your dream” utakaotolewa katika shule za Msingi na Sekondari nchini kwa kushirikiana na wataalam wa afya kutoka Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na mashirika ya binafsi ili kuokoa vijana na kulinda maadili ya Mtanzania.

Kwa upande wake Katibu wa shirika hilo, Romanus Dominicus alitoa wito kwa wazazi na walezi kuendeleza maadili katika Taifa kwani hakuna Taifa lililoendelea Duniani kwa kuharibu maadili na nidhamu ya watoto.

“Umefika wakati kwa mashirika mengine, wazazi, walezi na walimu kushirikiana kutoa elimu sahihi na salama kwa watoto wetu wa kike na wa kiume kuhusu madhara ya vitendo vya ngono na mimba za utotoni,” alisema Dominicus.

Dominicus aliongeza kuwa Shirika la WAN pamoja na wote wenye mapenzi ya dhati na watoto wa Tanzania wanahitaji kuwa na kizazi bora kitakachorithi na kumudu kuiendeleza Tanzania kwani kurithi nchi ni jambo jingine na kumudu kuiendeleza ni jambo jingine.

Agizo la kutoendelea na masomo kwa mtoto wa kike aliyepata ujauzito kwa shule za Msingi na Sekondari lilitolewa na Rais Magufuli mwezi June mwaka huu alipokuwa ziarani mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment