Thursday, 7 September 2017

WATUMISHI 193,000 KUPANDISHWA MADARAJA




WATUMISHI wa umma 193,000, watapandishwa madaraja katika mwaka huu wa fedha huku serikali ikiwa imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi yao na wazabuni mbalimbali baada ya kuhakikiwa.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri w a Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mahamoud Mgimwa, aliyetaka kujua ni lini malimbikizo ya madeni ya watumishi wa umma yataanza kulipwa.

Waziri Angella alisema watumishi wote wanaostahili kupandishwa madaraja watapandishwa katika mwaka huu wa fedha na kwamba, serikali haitamvumilia ofisa utumishi atakayezembea katika upandishaji wa madaraja kwa watumishi.

Aidha, Angella alisema muda wowote kuanzia sasa, watumishi wa umma wataongezewa nyongeza ya mwaka ya mishahara na kusisitiza kuwa, hakuna atakayeachwa.

Waziri huyo alionya kuwa, waajiri watakaochelewa kuwapandisha madaraja watumishi, watachukuliwa hatua kama ilivyotokea katika halmashauri za Bagamoyo, Kilombero na Temeke.

"Ikibidi tutawacheleweshea mishahara waajiri hawa ili waone uchungu wa kuwacheleweshea mishahara watumishi walio chini yao,"alisema.

Akijibu swali la msingi la Cosato Chumi (Mafinga Mjini-CCM), Waziri Angella alisema
serikali itaendelea kutoa nauli ya likizo kwa watumishi  wake mara moja katika kipindi cha miaka miwili.

Alisema nia ya serikali ni kuwapa motisha watumishi wa umma ili kuwaongezea morari ya kazi, lakini motisha inayotolewa inapaswa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi. Alisema serikali itaendelea kuboresha motisha kwa watumishi kadri uchumi utakavyoimarika.

Waziri Angella alisema likizo ya mwaka ni haki ya kila mtumishi wa umma na kwamba, hiyo imebainishwa katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 na Kanuni ya 97 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

No comments:

Post a Comment