Wednesday 4 November 2015

MAGUFULI AILETA DUNIA TANZANIA






Marais wanane, mawaziri wakuu kushuhudia akiapa
Kenyatta, Kagame, Museveni, Mugabe kuhudhuria
TB Joshua atua nchini kushuhudia, aelezea uchaguzi
Polisi yajipanga, ulinzi waimarishwa kila kona ya Jiji

Na Waandishi Wetu

RAIS Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kesho anakula kiapo na kukabidhiwa rasmi mikoba ya kuliongoza taifa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye amemaliza muda wake wa uongozi wa miaka 10.
Katika tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mamilioni ya Watanzania ndani na nje ya nchi, Dk. Magufuli ataapa huku akishuhudiwa na marais zaidi ya wanane kutoka mataifa mbalimbali duniani,  makamu wa rais, mawaziri wakuu na viongozi wengine wa ngazi za juu.
Sherehe hizo zitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa mamlaka husika, maandalizi yote yamekamilika huku ulinzi ukizidi kuimarishwa ili kuhakikisha amani na utulivu vinatawala.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda na wawakilishi wa ndani na nje watashiriki.
Miongoni mwa marais watakaohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Jacob Zuma (Afrika Kusini).
Wengine ni Joseph Kabila (DRC), Uhuru Kenyatta (Kenya), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Edgar Lungu (Zambia).
Taarifa hiyo imesema kuwa Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima huku Namibia ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Netumbo Nandi-Ndaitwah na kwa upande wa Serikali ya China , itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Tawala.
Nchi zingine ambazo tayari zimethibitisha kushiriki katika sherehe hizo na zitawakilishwa na makamu wa rais,  waziri mkuu,  spika au balozi ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius.
Nyingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.
Kwa upande wa wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda, waliothibitisha kushiriki ni Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika  (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuia ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

TB Joshua atua kushuhudia
MTUME TB Joshua wa Kanisa la Church of All Nations la nchini Nigeria, amewasili jijini Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kushuhudia kuapishwa kwa Dk. Magufuli.
Mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, TB Joshua alikwenda moja kwa moja Ikulu, kumsalimia Rais Jakaya Kikwete.
Katika mazungumzo yao, TB Joshua alimpongeza Rais Kikwete kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, ambao alisema ulifanyika kwa uhuru na amani.
Alimweleza kuwa kutokana na kufanikisha uchaguzi huo, anaondoka madarakani kwa furaha na amani na kuwaacha Watanzania wakimkumbuka daima.
Aidha, alimpongeza Rais Kikwete kwa kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpata Dk. Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano, ambaye alimwelezea kuwa ni Rais wa Baraka na Fanaka tele katika awamu hii mpya.

Polisi yaonya, yataka amani
JESHI la Polisi limewataka wananchi  kudumisha amani wakati huu, ambao Taifa linaingia kwenye tukio muhimu la kuapishwa kwa Dk. Magufuli.
Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Changoja, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, tukio hilo ni muhimu na kwamba, ulinzi umeimarishwa kila kona.
Aliwataka wananchi kuhakikisha amani iliyokuwepo wakati wa uchaguzi mkuu, inaendelea  hata siku zote, ikiwa ni pamoja na siku ya kuapishwa rais mteule.
Chagonja  aliwataka wananchi kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya aina yoyote, ambavyo vinaweza kuhatarisha  usalama wa raia na mali zao.
Aliwataka kujiepusha na maandamano  yanayopangwa kufanyika bila kufuata utaratibu, vurugu na ushabiki wa kisiasa na  kueneza uvumi usio wa kweli.
Chagonja aliwataka wananchi kuwa makini  na matumizi ya mitandao ya kijamii katika  kulinda amani ya nchi.
“Wananchi tuhakikishe tunaiweka nchi katika hali ya usalama kama ilivyokuwa kipindi  chote cha uchaguzi,” alisema.
Chagonja alisema jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama, vimejipanga kikamilifu  kuhakikisha usalama wa raia na mali zao  unaimarishwa.
Alisema polisi hawatasita kuchukua hatua kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachoonyesha viashiria vya uvunjifu wa  amani.
Akizungumzia maandamano ya CHADEMA, Chagonja alisema maandamano hayo ni batili na kwamba waliwasilisha maombi nje ya muda.
“Hatuoni haja ya kuwa na maandamano kwa sasa na kama chama kimojawapo kinaona hakijatendewa haki, kifuate sheria kwa maana kimepewa njia ya kufuata,’’ alisema.

No comments:

Post a Comment