Wednesday 4 November 2015

MAKAMISHNA ZEC WAKALIWA KOONI




NA MUSSA YUSUPH
MAKAMISHNA wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wametakiwa kuwajibika kwa kuwa sehemu ya kuharibika kwenye visiwa hivyo.
Pia, mamlaka za uteuzi zimeombwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maofisa wa tume hiyo kwa kusababisha kufutwa kwa uchaguzi.
Imesisitizwa kuwa, mvutano huo wa kisiasa unaweza kutatuliwa nchini pasipo kutegemea taasisi au mataifa ya kigeni.
Ikumbukwe kuwa, Oktoba 28 mwaka huu, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alisema baadhi ya wajumbe wa tume hiyo walirushiana makonde wenyewe kwa wenyewe na kutia dosari uchaguzi huo.
Hali hiyo ilijitokeza kufuatia wajumbe hao, kuweka mbele maslahi ya vyama  vya siasa na sio ya Wazanzibari.
Kwa mujibu wa taarifa ya awali kuhusu uchaguzi mkuu, iliyotolewa jana, Dar es Salaam na Timu ya Uangalizi ya Uchaguzi ya (TEMCO), Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Profesa Benson Banna, alisema bado uamuzi uliofanywa na ZEC, umeacha maswali mengi.
Alisema uamuzi huo umesababisha mijadala mikali kwa wadau na kuleta dukuduku kati ya vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi.
Profesa Banna alisema, vyama vya siasa vinapaswa kuheshimu mamlaka ya ZEC, kama yalivyo kwa mujibu wa sheria na Katiba.
Alisema vyama hivyo vinapaswa kuepuka kutoa kauli za kiuchochezi zinazolenga kuhatarisha amani na mshikamano nchini.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alibainisha kuwa, TEMCO ilishtushwa na tamko lililotolewa kwa umma na Chama cha CUF, Oktoba 26, mwaka huu.
Aliongeza kuwa tamko hilo ambalo halikusainiwa, lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka ‘CUF yashinda uchaguzi wa kihistoria Zanzibar.’
Alisema tamko hilo lilikuwa limeingilia mamlaka ya ZEC, hivyo ni wajibu kwa wanasiasa kuheshimu mamlaka ya tume hiyo kwa mujibu wa katiba.
Kufuatia hali hiyo, TEMCO imeuomba uongozi wa juu wa serikali ya Muungano, kufikiria na kuchunguza namna ya kusuluhisha mvutano huo unaoweza kuhatarisha amani.

TATHIMINI YA UCHAGUZI
Kwa mujibu wa ripoti za waangalizi wa TEMCO, ilibainisha kuwa, uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, unastahili hati safi ya uchaguzi huru na wa haki kwa kiwango cha daraja A.
Lakini, kutokana na mapungufu yaliyoainishwa na waangalizi, TEMCO imetoa hati ya daraja B ya uchaguzi huru wenye ulakini, kutokana na uwepo wa baadhi ya mapungufu.
Baadhi ya mapungufu yaliyotajwa na TEMCO ni kutoruhusiwa kuwepo kwa mgombea binafsi, uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutokupiga kura kwa Watanzania waishio nje ya nchi.
Profesa Banna alisema uchaguzi ulisimamiwa vizuri na matokeo yake yanaakisi matakwa ya wapigakura.
Alisema NEC ilitekeleza majukumu yake kwa uweledi, uchapakazi na uzalendo na kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na uzoefu iliyoupata NEC kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, inapaswa kuanza maandalizi ya upigajikura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuzingatia uboreshaji uliofanyika kwenye daftari la wapigakura.
Aidha, Profesa Banna, ameisisitiza tume hiyo kuendelea kuboresha daftari la wapigakura, hususan baada ya baadhi ya watu kudai kutoyaona majina yao kwenye daftari hilo.

MITANDAO YA KIJAMII
Katika kuangazia mchango wa mitandao hiyo kwenye uchaguzi, serikali imeombwa kuchukua hatua zitakazosaidia utendaji bora wa mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi.
Hatua hizo ni pamoja na kusimamia na kuongeza kasi ya udhibiti wa taarifa za kiuchochezi kwa kuepuka upotoshaji wa habari utakaoweza kuharibu mchakato wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa Profesa Banna, ni muhimu kuchukua hatua za kuimarisha asasi za makuzi ya vijana kwa lengo la kurekebisha tabia.
“Taasisi zinazohusika na malezi ya vijana ni muhimu zikawafunza vijana wawe na subira, wastahimilivu na wawajibikaji,” alisisitiza mhadhiri huyo.
Taasisi hiyo kinara katika masuala ya tafiti na usimamizi wa uchaguzi nchini, ilivitaka vyama vya siasa kuchukua hatua zaidi katika kujenga demokrasia na kuelekeza malalamiko yao kupitia njia muafaka za Kimahakama.

No comments:

Post a Comment