Thursday 19 November 2015

TOFAUTI ZA KISIASA ZANZIBAR NI DONDA NDUGU


RAIS Dk. Ali Mohamed Shein
RAIS mstaafu Amani Abeid Karume


Na Mwandishi Maalumu
KIMYA kinachoendelea cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya uamuzi wake wa kufuta matokeo yote ya Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu na propaganda zinazoendelea miongoni mwa wanasiasa, wanasheria na watu mashuhuri, zinaashiria mpasuko mwingine mkubwa wa kisiasa visiwani humo.
Hali hiyo ya mgogoro wa sasa inayatia hitilafu kubwa mafanikio ya kupigiwa mfano ya muafaka wa kisiasa Afrika, uliofikiwa miaka saba iliyopita, baada ya mazungumzo baina ya viongozi wawili wa vyama vya siasa, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar wakati huo, Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye baadae alikuja kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Suala muhimu ambalo limekuwa likipata majibu tofauti ni namna gani Zanzibar inaweza ikatoka hapa ilipo kuhusiana na suala la uchaguzi, wakati sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tanzania Bara) imeanza kusahau makovu yaliyotokana na uchaguzi huo.
Tofauti ya majibu kutokana na suala moja inatokana na namna suala lenyewe na namna ambavyo wanaopaswa kulijibu wamekuwa wakilizungumzia. Jambo linaloonekana wazi wazi ni athari ya mitazamo ya kisiasa miongoni wa wazungumzaji wote, kuanzia kwenye Tume, wanasheria na bila ya shaka wanasiasa wenyewe.
Katika sababu tisa zilizotajwa na Mwenyekiti wa Tume, sababu ya pili ilisomeka na kusikika kama ifuatavyo:
“Ni dhahiri baadhi ya wajumbe badala ya kuwa makamishna wa Tume, wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao. Na ikumbukwe kuwa vipo vyama vingi zaidi, ambavyo havikupata fursa ya kuwa na makamishna ndani ya Tume na vimeshiriki katika uchaguzi huu mkuu”.
Athari za siasa ndani ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zilionekana pale mambo yalipokuwa yanakwenda vibaya kiasi ambacho kila mtu aliweza kushuhudia ukiukwaji wa wazi wa sheria za uchaguzi huku wengine wakiwa tayari kupigana na kufanya kila lililo ndani ya uwezo wao na nje ya uwezo wao, ilimradi kinachofanyika kitaleta maslahi ya kisiasa kwa chama chake.
Kwa mfano, kulikuwa na makosa mengi ya kubadilisha matokeo kwa kutumia wino maalumu wa kufutia na pia kwa kupandishia tarakimu za kura kwa baadhi ya wagombea.
Imetokezea katika jimbo la Kojani, mgombea alipata kura 1,003, lakini tarakimu ya kwanza ilirukwa (iliachwa) kwa makusudi kupunguza kura zake na kuwekwa 0003. Mhusika alipoulizwa alikubali kuwa alifanya kosa, lakini aliomba msamaha eti kwa kuwa lilikuwa ni kosa la kibinadamu.
Makosa ya aina hiyo yalionekana kwenye maeneo mengi Unguja na Pemba, mbali na yale ya kupatikana karatasi mbili au tatu za mpigakura, zilizokunjwa kwa pamoja ndani ya sanduku la kupigia kura, zikitoa taswira ya wazi kwamba zilipigwa na mtu mmoja. Muhimu zaidi ni kwa karatasi zote hizo kumpigia kura mgombea mmoja.
Lakini kulikuwa na taarifa ya mtu mmoja kukamatwa na karatasi za kupigia kura na alikuwa ameshikiliwa na polisi, kesi iko mahakamani.
Pia kuna ushahidi kwamba kuna watu Pemba, ambao wakati wa kupigakura, walikuwa wanaranda na karatasi za kupiga kura kwenye mikoba wakiwa tayari kulipa sh. 50,000 kwa karatasi moja waruhusiwe kuziingiza karatasi zao kwenye visanduku vya kupigia kura.
Kinachoshangaza ni pale wakati hoja muhimu za aina hiyo zinapowasilishwa kwenye Tume, makamishna kutoka chama kimoja cha siasa kwa pamoja wanakataa katakata kulijadili suala hilo, huku wakisisitiza kuendelea kuhesabu kura hata kama kuna mapungufu ya msingi yameonekana na kwamba masuala ya aina hiyo yatajadiliwa tu baadae, baada ya Tume kumtangaza mshindi.
Hili linatosha kusema kuwa tatizo la siasa ni la msingi na inakuwa vigumu kuweza kulipatia ufumbuzi wa kudumu. Wengi miongoni mwa wananchi wa Zanzibar waliamini kwamba muafaka wa kisiasa ungekuwa ndio ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
Licha ya Serikali ya CCM na hasa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mvumilivu sana kisiasa, siasa za upinzani zimeendelea kuonekana bayana ndani ya serikali anayoiongoza.
Bado inakumbukwa hali ya mvutano wa kisiasa ndani ya Bunge la Katiba na hata kwenye Baraza la Wawakilishi lililopitisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2015/2016. Watendaji wengi ndani ya serikali pia wanaonekana kuathiriwa na hali hiyo.
Miongoni mwa wazungumzaji wa suala hili waliovuta hisia za wafuasi wa upinzani ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, ambaye alifutwa wadhifa wake huo kutokana na mwelekeo wake kisiasa.
Othman naye licha ya kuwa sasa anajitambulisha kama mwanasheria wa kujitegemea, hakusalimika na siasa. Wakati alipokuwa kwenye Bunge la Katiba, alionekana kusahau jukumu na wajibu wake wa kazi na kujiingiza kichwa kichwa kwenye saisa za upinzani.
Kabla ya sakata hilo la uchaguzi, Othman amekuwa akihudhuria matukio mbali mbali ya kisiasa akionyesha wazi wazi msimamo wake kisiasa. Mwanasheria kama huyu hupoteza hadhi na sifa yake kutokana na kusahau fani yake na kujiingiza kwenye siasa. Ingependeza iwapo angekuwa muwazi wakati anapoanza kutoa maelezo yake kwa kusema kuwa anatoa maelezo hayo akiwa ni mfuasi wa kundi linalotetea Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Huu ni utaratibu wa kawaida katika masuala ya kisheria kutangaza maslahi binafsi ‘to declare interest’ kabla ya kuingia kwenya mada husika. Usipofanya hivyo, unapoteza sifa na hadhi ya kuamua chochote baina ya pande mbili husika.
Kwa mfano, kwa wale wanaohudhuria vikao vya zabuni, wenye kampuni yao, ya jamaa zao au hata wanaowafahamu tu, wanaoomba kazi hutakiwa kutoshiriki kwenye maamuzi kabla ya kujitangaza kuwa wao wana uhusiano na wanaojadiliwa, na maamuzi ya wajumbe ndiyo yatakayofuatwa ama wabakie kwenye mjadala au waondoke. Hii ni kusema kuwa Othman Masoud amepoteza sifa za kulizungumzia suala la Zanzibar kama mwanasheria. Anaweza kufanya hivyo akiwa UKAWA.
Matatizo ya aina hiyo yameonekana pia kwa wanasheria wengine kama vile Hamid Mbwezeleni. Ingawa hakusema bayana, lakini ilionekana wazi kuwa alikuwa mfuasi wa CCM au uchambuzi/ maoni yake yaliegemea kuisaidia CCM.
Tukirejea kwenye hoja ya msingi ni kwamba uchaguzi umekwama. Sasa swali gumu ni kuwa ‘tutatokaje hapo tulipo?’
Hoja mbili ndizo zinazoangaliwa; kuendelea kutangaza matokeo ambayo Mwenyekiti wa Tume amesema kwa kauli yake kuwa ameridhika uchaguzi haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo kwa uwezo alionao alitangaza rasmi kwamba uchaguzi huo na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurejea uchaguzi huo.
“…..kwa kuzingatia hayo na mengine ambayo sijayaeleza, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”. Ilisomeka taarifa ya Mwenyekiti iliyotiwa saini na yeye mwenyewe.
Mengi yamezungumzwa kutokana na taarifa hiyo; wapo wenye kusema Jecha hana uwezo wa kisheria wa kutoa tamko hilo na wengine wanasema anao uwezo wa kufanya hivyo.
Wapo wanaodai Mwenyekiti huyo wa Tume alilazimishwa na CCM kutoa tamko hilo. Lakini taarifa za ndani zinasema kuwa baada ya tamko hilo Tume ilikaa kuliidhinisha na ndipo likathibitishwa uhalali wake kwa kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la Serikali.
Wapo wanaosema kuwa Mwenyekiti alikuwa na uhalali wa kisheria wa kutoa tamko hilo kwani yeye na Mkurugenzi wa Tume ndio waliopewa dhamana ya kutoa matamko ya Tume.
Tafsiri ya sheria ndiyo tatizo linaloonekana kwenye mjadala huu. Kimsingi Tume ndiyo yenye maamuzi ya mwisho katika suala hili. Uamuzi wa Tume kama ulivyotolewa na Mwenyekiti au Jecha kama wengine wanavyotamka ni kurejea uchaguzi. Tukubali kuwa sehemu muhimu na maalumu tutakapopata tafsiri ya sheria ni kwenye mahakama.
Kwa kujibu tutatokaje hapa tulipo, ni ama kuendelea na mchakato wa uchaguzi mwingine au kama ilivyotangaza Tume au kwenda mahakamani kupata tafsiri ya sheria. Kwa bahati mbaya au bahati nzuri, uamuzi wa Tume hauhojiwi na mahakama yoyote duniani.
Hata hivyo, ifahamike wazi kwamba si uamuzi wa mahakama wala wa Tume ambao utaivusha Zanzibar na mgogoro wa kisiasa. Lolote miongoni mwa hayo halitaiweka Zanzibar salama na mgogoro wa kisiasa. Wapo waliopatwa na hofu kwamba hata maamuzi ya mahakama za Zanzibar ama yamekuwa yakitolewa kwa misingi ya fedha au kisiasa.
Itakumbukwa kuwa moja kati ya masuala ambayo yalimpa changamoto Rais Kikwete katika kuupatia ufumbuzi mpasuko wa kisiasa Zanzibar wakati alipokuwa anaingia madarakani mwaka 2005, ni kiasi kikubwa cha Wazanzibari wenyewe kutoaminiana.
Shida hiyo itaendelea kuitafuna Zanzibar na tatizo hilo litaendelea kwa miaka mingi ijayo. Kwa hivyo ni dhahiri kuwa suala la kuaminiana miongoni mwa wadau wa siasa Zanzibar ni la kwanza katika kuiondoa Zanzibar katika mkwamo huu wa kisiasa.

No comments:

Post a Comment