KATIBU
Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi John Ndunguru, amewasimamisha kazi watumishi
tisa wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, kwa ubadhirifu wa fedha
za umma.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, mjini hapa, Mhandisi Ndunguru,
alisema kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, kumetokana na tuhuma za ubadhirifu
wa mali za umma.
Alisema
tuhuma hizo zilibainika wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa, aliyoifanya
hivi karibuni mkoani hapa.
Mhandisi
Ndunguru alisema mkoa uliunda kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma hizo na
kubaini kuwa, watumishi hao wamefanya udanganyifu katika mikataba mbalimbali na
kuisababishia serikali hasara.
Alisema
ubadhirifu uliofanywa na watumishi hao ni manunuzi hewa ya shajara yenye thamani
ya sh. milioni nne, vipuri milioni nane pamoja na matumizi mabovu ya fedha za
serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Alitaja
ubadhirifu mwingine waliofanya watumishi hao ni kuuza majengo ya Kigodeco na
Mibox kwa bei ya chini, ambayo ni sh. milioni 370, badala ya sh. milioni 470.
"Kamati
imefanya kazi nzuri ya uchunguzi wa awali, hivyo kuanzia sasa namsimamisha kazi
Willyfred Mwita, ambaye ni Ofisa Mipango, Emanuel Mkwe, ambaye ni mwanasheris,
Boniface William, ambaye ni Mhandisi na Mussa Igugu, Ofisa Biashara.
Wengine
ni Elimboto Zakaria, ambaye ni Mkaguzi wa Ndani, Leonard Nzilailunde, ambaye ni
Ofisa Misitu, Shida Tadei, ambaye ni Ofisa Ugani, Bawili Mkoko, ambaye ni Mhasibu na Omary Lubibi, Fundi Mkuu wa
Magari.
Ndunguru
alisema amewasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi dhidi yao
uendelee kufanyika kwa kina na maofisa kutoka TAMISEMI, ambao watawasili mkoani
humo kwa ajili ya kazi hiyo.
Aidha,
amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuhakikisha mali zote za serikali
zilizouzwa kinyume na taratibu za kisheria, zinarudi kwenye halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment