CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM), kimeitaka serikali ya awamu ya tano, kuendelea kuwasaka watumishi
hewa walioisababishia hasara kubwa ili wachukuliwe hatua, ikiwemo kuwaamuru
walipe fedha hizo zifanye kazi zingine kwa manufaa ya wengi.
Kimesema
kitaendelea kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika jitihada zake za
kuwaletea Watanzania maisha bora kwa kuwabana wabadhirifu, wezi wa mali za umma
na hakitakaa kimya atakapojitokeza mtu wa kumzuia.
Kimesema
viongozi wa juu wa CCM watazunguka nchi nzima kuhakikisha watendaji wa ngazi
zote katika Chama, wanafanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu kama
inavyoeleza misingi ya CCM pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani.
Pia,
kimesema hakitakaa kimya kuangalia wachache wakidhulumu haki za Watanzania kwa
sababu kimeingia nao mkataba wa kuwatumikia kwa miaka mitano kupitia Ilani hiyo
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Akizungumza
jana, wilayani Babati, mkoani Manyara, kwenye mkutano wa kwanza wa hadhara,
Msemaji Mkuu wa CCM Taifa, Christopher Ole Sendeka, alisema CCM imepewa dhamana
na Watanzania kuiongoza nchi na itafanya hivyo bila kuchoka.
Alisema
tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, inayoogozwa na CCM,
tayari mambo makubwa yamefanyika na bado yataendelea kufanywa kwa nguvu zote na
kwamba kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ inafanywa na Rais Magufuli kwa vitendo.
Ole Sendeka
alisema CCM inatuma salamu kwa baadhi ya watu wanaoendelea kueneza siasa ya
chuki, dharau, matusi kama ile ya wakati wa uchaguzi mkuu kwamba, waache kwa
sababu hawana nafasi kwa serikali ya awamu hii, iliyokusudia kuwatumikia Watanzania
bila ubaguzi wa kiitikadi.
"CCM ni
ya Watanzania, tunaanza zoezi la nchi nchi nzima kuwaeleza wananchi kuwa yapo
maisha baada ya uchaguzi, ambayo ndio CCM tunayaishi sasa. Tunachapa kazi kama
tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi na tutaendelea kufanya hivyo, wanaokosoa
utendaji wetu si wazalendo," alisema.
Aidha,
alisema urais wa Dk. Magufuli hauna ubia na kiongozi yeyote wa nchi hii na
kwamba, anatimiza wajibu wake kwa misingi ya sheria na kanuni za nchi.
Alitumia
fursa hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kuiunga mkono CCM na serikali yake,
ili iendelee kutekeleza majukumu yake kwa umma na wawapuuze wanaokosoa juhudi
hizo kwa maslahi binafsi.
Awali,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa Mkoa wa Kigoma, ambaye aliambatana na Ole
Sendeka, kwenye ziara hiyo, Kilumbe Ng'enda, alisema lengo la ziara hiyo ni
kuwashukuru wananchi wa Kata ya Bashneti kwa kuichagua CCM baada ya kuwa chini
ya upinzani kwa miaka 15 iliyopita.
Katika
matokeo ya uchaguzi uliopita, kata hiyo ilimchagua Jovita Mandoo wa CCM kuwa diwani
kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 15, ambapo tayari ameanza kazi ya kujenga
ofisi ya kata.
Katika
kuunga mkono juhudi hizo, Ole Sendeka alichangia mabati ili kukamilisha ujenzi
huo.
Leo, Ole
Sendeka anaendelea na ziara yake mkoani humo kwa kukutana na viogozi wa wilaya
na mkoa wa Chama ili kuzungumza nao mambo mbalimbali ya kukiimarisha Chama.
No comments:
Post a Comment