Thursday, 18 August 2016
BOSI WA ZAMANI NIDA, WENZAKE SABA KORTINI
NA FURAHA OMARY
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake saba, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 27, yakiwemo ya kuisababishia hasara mamlaka hiyo ya zaidi ya sh.bilioni 1.16.
Mbali na mkurugenzi huyo, washitakiwa wengine waliofikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ni Meneja Biashara, Avelin Momburi, Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage na kurudishwa rumande hadi Agosti 31, mwaka huu, kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kutoa dhamana kwa washitakiwa Maimu, Mwakatumbula, Ndege, Ntalima, Sabina na Kayombo, kwani wanatakiwa kuwasilisha maombi Mahakama Kuu.
Washitakiwa Momburi na Makani wanatakiwa kurudi mahakamani hapo kesho ili kujua hatima ya maombi yao ya dhamana, yaliyowasilishwa na mawakili wao kutokana na mashitaka yanayowakabili kutoangukia katika sheria ya uhujumu uchumi.
Maimu na wenzake walifikishwa mahakamani hapo saa tatu asubuhi, wakiwa katika magari mawili ya TAKUKURU, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kusababisha ndugu na jamaa zao waliofurika mahakamani hapo kuangua vilio.
Ilipotimu saa 6.30 mchana, Maimu na wenzake, ambao walikuwa wakitokea kituo cha polisi walikolala tangu juzi kwa mujibu wa wakili wao, Jamhuri Johnson, walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mwijage, ambapo jopo la mawakili wa serikali, likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa, akishirikiana na Mawakili kutoka TAKUKURU, Janeth Machulya, Leonard Swai, Joseph Kiula na Fatuma Waziri, liliwasomea washitakiwa hao mashitaka hayo.
Kabla ya kuanza kuwasomea mashitaka yanayowakabili, Hakimu Mwijage aliwaeleza washitakiwa hao kwamba, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ambayo husikilizwa na Mahakama Kuu, labda Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) atoe kibali kwa mahakama ya chini kusikiliza, hivyo kwa kuwa DPP hajatoa kibali hicho, hawatatakiwa kujibu lolote.
Mawakili hao wa serikali waliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya kutumia madaraka vibaya, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri, kusababisha hasara ya jumla ya sh. 1,169,352,931 na kula njama.
Katika shitaka la kwanza, Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15 hadi 19, 2010, katika makao makuu ya NIDA, yaliyoko wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa utumishi wa umma kwa nafasi katika NIDA, wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00, bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, ambayo ni kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya sh. 3,969,000.
Maimu na Mwakatumbula pia wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013, katika makao makuu hayo, katika utekelezaji wa majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya sh. 106,346,000.
Mkurugenzi huyo wa zamani wa NIDA na Mwakatumbula, wanadaiwa Juni 20, 2014, katika makao makuu hayo, walipitisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000, kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya sh.42,471,000.
Aidha, Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo ya sh. milioni sita, kwa GIL bila ya kupiga mahesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya sh.14, 661,676.76.
Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015, katika makao makuu hayo ya NIDA, kwa kupitisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni, ambapo waliisababishia NIDA hasara ya sh.167,445,676.76.
Mshitakiwa Ndege anakabiliwa na mashitaka ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri, ambapo kati ya mashitaka hayo, anadaiwa Aprili 16, 2012, katika makao makuu ya NIDA, akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, ambayo imeingia mkataba na NIDA wa kutoa huduma za bima, alitumia kwa nia ya udanganyifu kwa mwajiri wake NIDA, aliwasilisha hati ya malipo yenye taarifa za uongo kwamba, kampuni yake inastahili kulipwa sh. 22,582,281, kwa huduma za bima iliyoitoa huku akijua taarifa hizo ni za uongo na zina lengo la kumdanganya mwajiri wake.
Momburi, Mwakatumbula na Ntalima wanadaiwa kati ya Februari 22 na Aprili 17,2012, katika makao makuu hayo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo ya sh.22,582,281 kwa kampuni ya Aste Insurance Brokers, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya kiasi hicho.
Maimu, Mwakatumbula na Ntalima pia wanakabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, wakidaiwa kupitisha malipo ya bima kwa kampuni ya Aste, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya viwango mbalimbali vya fedha.
Mkurugenzi huyo wa NIDA, Mwakatumbula, Ndege na Ntalimwa wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Januari 4,2013, katika makao makuu ya NIDA, waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya sh.55,312,800.
Aidha, Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kati ya Januari 29 na 30, 2013, katika makao makuu hayo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo ya Dola za Marekani milioni mbili, kwa IRS CORPORATION BERHAD, kwa mapendekezo ya utaratibu mpya wa haraka wa upatikanaji wa vitambulisho na vifaa bila ya kufanya marekebisho ya mkataba ulioko kati ya NIDA na kampuni hiyo, hivyo kuifanya IRIS kupata faida ya dola hizo.
Pia, Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kupitisha malipo kwa kampuni hiyo ya IRIS ya viwango mbalimbali, hivyo kuifanya ipate faida.
Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni mosi na 6, 2013, katika makao makuu hayo, kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la kutumia nyaraka za uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri.
Washitakiwa Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni 4 na 6,2013, katika makao makuu hayo, waliisababishia hasara NIDA ya sh.45,515,961.
Maimu na Sabina wanadaiwa kati ya Agosti 3, 2010 na Novemba 7,2011, katika makao makuu ya NIDA, wakati wakitekeleza majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya na kuiwezesha GIL kupata faida
ya sh. 901,078, 494 na kuisababishia NIDA kupata hasara ya kiasi hicho.
Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka, Wakili Mbagwa alidai mashitaka yanayowakabili washitakiwa wote yanadhaminika kwa mujibu wa sheria, lakini mahakama yenye mamlaka ya kutoa dhamana ni Mahakama Kuu, kwa kuwa kiwango kilichoko katika hati ya mashitaka ni zaidi ya sh. milioni 10.
Kwa upande wa wakili wa utetezi, Michael Ngalo, alidai washitakiwa wao sita ambao wana mashitaka ya uhujumu uchumi, watawasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Kuhusu washitakiwa Momburi na Makani, mawakili wao akiwemo wa Jamhuri, walidai wanastahili kupatiwa dhamana na Mahakama ya Kisutu kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanaangukia katika sheria ya uhujumu uchumi.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Mbagwa alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, hivyo mahakama hiyo ya Kisutu haiwezi kuwapatia dhamana.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mwijage alisema hatima ya dhamana ya Momburi na Makani itajulikana kesho, atakapotoa uamuzi juu ya maombi yao.
Hakimu Mwijage alisema washitakiwa Maimu, Mwakatumbula, Ndege, Ntalima, Raymond na Kayombo, wanapaswa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa makosa yao yanaangukia chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi. Alisema kesi kwa washitakiwa wote itatajwa Agosti 31, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment