Thursday, 18 August 2016

WALIMU DAR WATAFUNA FEDHA ZA ELIMU BURE

WAKATI  serikali  ikiendelea na mapambano dhidi ya watumishi hewa, ufisadi mkubwa umebainika kufanywa na  baadhi ya walimu  wa shule za msingi na sekondari, kwa kuandikisha majina ya wanafunzi hewa ili kujipatia fedha za ruzuku ya elimu bure inayotolewa na serikali.

Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imekuwa ya kwanza nchini kuanika ufisadi huo, tangu serikali ya awamu ya tano chini  ya Rais Dk. John Magufuli ilipoanza utekelezaji wa sera ya elimu bure.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi, alisema uchunguzi uliofanyika umebaini majina ya wanafunzi hewa 3,462 katika shule za msingi  68 wilayani humo.

Kiasi hicho cha wanafunzi ni sawa na shule moja ya msingi, ambapo serikali ilikuwa ikitoa ruzuku hewa ya elimu bure kwa shule moja hewa yenye wanafunzi hewa wilayani humo.

Hapi alisema kwa upande wa sekondari, imebainika kuwepo majina ya wanafunzi hewa  2,534,  ambapo shule zilizobainika kuwa na wanafunzi hao ni  22.

Kama ilivyo kwa wanafunzi hewa walioandikishwa kwenye shule za msingi, dadi hiyo ya wanafunzi inaweza kutosha shule moja ya sekondari.

Hapi alisema uchunguzi umeonyesha kuwa, katika kipindi cha miezi mitatu, walimu hao waliitia serikali hasara ya zaidi ya sh. milioni 70.

Kutokana na sakata hilo, Hapi amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo,  kuwavua mara moja nyadhifa za ukuu wa shule kwa upande wa shule za msingi.

“Kwa upande wa shule za sekondari, kwa kuwa wakuu wa shule hizo wako  chini ya  Katibu Tawala wa Mkoa,  tumemwandikia barua ili aweze kuwavua nafasi hizo mara moja kwa kosa la udanganyifu wa takwimu,”alisema Hapi.

Alibainisha kuwa pia ofisi yake pia imeiandikia Tume ya Utumishi wa Walimu kupitia kwa mkurugenzi,  ambaye ndiye mwajiri wao,  kuhakikisha hatua kali zaidi zinachukuliwa dhidi ya walimu hao.

“Lakini kubwa zaidi ni kwamba, walimu hao wote watatakiwa kurejesha fedha zote walizochukua kupitia majina hayo hewa katika mishahara yao na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,”alibainisha Hapi.

Alisema alibaini mchezo huo mchafu, wakati akitekeleza agizo  la Rais Dk. John Magufuli, alililotoa hivi karibuni la kuwataka wakuu wa wilaya nchini kufuatilia kiundani  matumizi ya ruzuku ya sh. bilioni  18.8, ambazo serikali inatoa kwa shule zote nchini kila mwezi, ili kufanikisha sera ya elimu bure.

“Kwa wilaya yangu ya Kinondoni, niliagiza uhakiki ufanyike wa wanafunzi wote waliopo shuleni, darasa kwa darasa, shule hadi shule, tena kwa majina halisi ya wanafunzi. Ndipo nilipogundua kwamba kuna udanganyifu mkubwa unaofanyika kwa walimu kuongeza majina ya wanafunzi hewa, ili serikali inapotoa fedha za ruzuku, walimu wanazichukua kupitia majina hayo bandia,”alisema Hapi.

Aliongeza: “Hatutakuwa na huruma na mwalimu yeyote atakayefanya udanganyifu wa takwimu na atakayeghushi takwimu na kufanya udanganyifu kwa lengo la kujipatia fedha za elimu bure kinyume cha sheria. Tutamshughulikia kisawasawa. Ninaonya walimu waache mara moja.”

Alisema inasikitisha kuona Rais Dk. Magufuli anahangaika kutafuta fedha  ili wanafunzi wasome bure na kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi, lakini walimu wasio waaminifu wanathubutu kujinufaisha na fedha hiyo kwa njia za udanganyifu.

Pia, alisema ameagiza nafasi  za walimu hao wakuu  68, wapewe walimu wa kuu vijana, wanaokidhi sifa na wenye uwezo wa kuendana na kasi ya serikali ya  awamu ya tano.

Baadhi ya shule  za msingi zilizotajwa kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi hewa ni Msisiri B, iliyoko kata ya Mwananyamala, yenye  wanafunzi hewa 395, ambapo Mwalimu Mkuu ni Sophia Zewe na kiasi cha fedha zilizopotea ni sh. 636,345, kwa kipindi cha miezi mitatu.

Shule zingine ni Msisiri, chini ya Suzana Orege, wanafunzi hewa 357 (sh.575,127), Upendo, Mbezi, Mwalimu Mkuu, Yusuph Zanny, wanafunzi hewa 273 (sh.439,803), Msewe,  Mwalimu Mkuu, Rehema Ramole, wanafunzi hewa  267 (sh.430,137) na  Adrisa Abdul Wakili, Mwalimu Mkuu, Chiza Abel iliyobainika kuwa na wanafunzi hewa  187 (sh. 301,257).

Zingine, ambazo wanafunzi hewa wamebainishwa kwenye mabano ni  Golani, Kimara (174), Mchangani, Makumbusho (149), Makuburi Jeshini (145), Kawe A (109), Makongo (106) na Umoja Mabibo (104).
Shule zingine zina wanafunzi hewa chini ya 100 hadi mmoja.

Kwa upande wa baadhi ya shule za  sekondari ni Hananasifu, Kinondoni yenye wanafunzi hewa 154,  Boko (74), Bunju A (155) na Goba Mpakani (42).

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia amewavua madaraka walimu wakuu 12, wa shule za msingi, wakuu 11 wa shule za sekondari pamoja na waratibu wa elimu kata 10, kwa tuhuma kuwasilisha tarifa za uongo za idadi ya wanafunzi.

Kihamia amewavua madaraka walimu hao kutokana na kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 27.2, kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya mkurugenzi,katika shule za msingi 12, wapo wanafunzi hewa 907, ambao walipelekewa fedha za elimu bure sh. milioni 3.9 na katika shule 11 za sekondari, kulikuwa na wanafunzi hewa 942, ambao walipelekewa sh. milioni 23.3.

Taarifa hiyo imezitaja shule za msingi kuwa ni Azimio, Kimandolu, Magereza, Maweni, Moshono, Naura, Njiro Hill, Okrkeryani, Salei, Sokoni I, Terati na Wema.

Shule za sekondari ni Arusha Day, Kinana, Baraa, Kaloleni, Kimaseki, Korona, Moshono, Naura, Ngarenaro, Olorieni na Suye.

No comments:

Post a Comment