SERIKALI imevitaka vyuo vikuu 31 kati ya 81, vilivyopokea fedha za wanafunzi hewa 2,192, kurejesha sh. 3,857,754,460, ndani ya siku saba, ambazo ni gharama ya malipo ya wanafunzi hao waliopata mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HSELB), katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016.
Aidha, kamati ya uchunguzi ya kuhakiki wanafunzi wa elimu ya juu, ambayo inashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), imesababisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE), kumsimamisha mhasibu wa chuo hicho, huku maofisa kutoka HESLB wakipewa barua ya kuhojiwa kwa mashaka ya kuhusika na utafunaji wa pesa hizo.
Akizungumzia taarifa ya kamati hiyo ya kuhakiki wanafunzi kwenye Taasisi za Elimu ya Juu nchini jana, Dar es Saalam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Jocye Ndalichako, alisema uhakiki huo umefanywa kwa miezi miwili, kati ya Mei na Julai,mwaka huu, ambapo ilifanikiwa kuhakiki vyuo 31.
Profesa Ndalichako alisema mchakato wa kuhakiki wanafunzi hao endapo wana uhalali wa kupata mikopo hiyo, umebaini kuwa kuna madudu, ambapo imebainika baadhi ya wanafunzi waliohitimu, lakini bado wanaendelea kupokea fedha hizo, huku wengine waliofukuzwa kwa kushindwa masomo tangu mwaka 2013/2014, bado wanalipwa hadi mwaka 2015/2016.
Alisema serikali inatarajia kuchukua hatua za kinidhamu kwa wote waliohusika kufanikisha malipo kwa wanafunzi, ambao hawapo vyuoni na kwamba, hatua hiyo itawahusisha wafanyakazi wa HSELB na vyuo husika.
Waziri huyo aliongeza kuwa, uchunguzi zaidi utafanyika kwa miaka iliyopita ili kubaini fedha za mikopo, ambazo zimelipwa kwa watu wasiostahili, ambapo hatua hiyo inatokana na matokeo ya uchunguzi huo kuonyesha kuwepo kwa wasiwasi wa kuwepo idadi kubwa ya wanafunzi waliokwishamaliza masomo kuendelea kulipwa.
"Mchakato wa kuanza kuhakiki wanafunzi hao ulifanyika kwa awamu tatu kwa kila taasisi ili kuwapa nafasi wanafunzi, ambao hawakuweza kujitokeza kwa uhakiki awamu ya kwanza au ya pili, kujitokeza katika awamu zilizofuata za uhakiki kwenye chuo husika,"alisema.
Aliongeza kuwa katika awamu ya kwanza, wanafunzi 2,763, hawakujitokeza kwa uhakiki, ambapo Julai 18,mwaka huu, taarifa ya kuhakiki wanafunzi hao ilitolewa na orodha ya majina ya wahusika.
Alisema katika awamu ya pili na ya tatu, jumla ya wanafunzi 571, walijitokeza kuhakikiwa katika vyuo vyote 31 hadi hatua ya mwisho ya uhakiki ilipokamilika kwa taasisi hizo, ambapo timu hiyo ya uchunguzi ilibaini kuwepo kwa wanafunzi 2,192, ambao hawakujitokeza kuhakikiwa.
Alisema uwepo na uhalali wa wanafunzi hao 2,192, haukuweza kuthibitishwa, hivyo uhakiki wa malipo hayo umesababisha hasara kwa serikali ya sh.3,857,754,560 kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
"Miongoni mwa sifa na vigezo vya kupata mkopo katika HESLB ni ufaulu wa masomo ya mwanafunzi, hivyo mchezo wa udanganyifu wa matokeo ya masomo, ambapo unakuta wanafunzi wameshindwa kufaulu mitihani yao, wanabadilisha matokeo halisi," alisema.
Profesa Ndalichako alitoa mfano kwa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), ambacho kimekuwa na jumla ya wanafunzi 13,972, ambao wananufaika na mikopo huku 350 hawakuhakikiwa na sh.70,438,635 zimelipwa kwa wasiohakikiwa.
"Wanafunzi 16,535 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wananufaika na mikopo hii, lakini 364, hawajajitokeza kuhakikiwa, ambapo sh.460,963,550 zimelipwa kwa wasiojitokeza kuhakikiwa,"alisema.
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), wanafunzi 6,227 wananufaika huku 235 hawajahakikiwa na sh.387,625,650 zimelipwa kwa wanafunzi hao.
Alivitaja vyuo vingine, ambavyo vimekumbwa na sakata hilo kuwa ni Chuo Kikuu cha Usimamizi wa fedha(IFM), Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Saalam (DUCE), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU),
Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha(RUCU), Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT-Mwanza).
Vingine ni Chuo Kikuu cha Arusha(UOA), Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE-DSM), Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (SEKOMU), Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU),
Chuo Kikuu cha Kiislamu (MUM-Morogoro), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana-DSM (SJUT-DSM), Chuo Kikuu cha Jordani (JUCO-Morogoro).
Vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Ufundi Arusha(ATC), Chuo Kikuu cha Mount Meru (MMU-Arusha), Chuo Kikuu cha Makumira-Arusha (TUMA), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU),Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT-Arusha), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Uhasibu Arusha (IAA), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT-Mbeya) na Chuo Cha Elimu ya Biashara(CBE-Dodoma).
Mchungunzi Mkuu kutoka TAKUKURU,Abubakar Msangi, alisema baadhi ya wanafunzi hao walikuwa wamepewa fedha hizo za mkopo, ambapo wengine wamehitimu masomo yao muda mrefu na bado walikuwa wakiendelea kupewa fedha hizo.
Msangi alisema uchunguzi huo pia umebaini kuwa orodha ya majina yaliyokuwa yakipewa malipo ya mikopo hiyo ni yale yale, ambayo yamekuwa yakitolewa kutoka vyuo husika na ndio hayo hayo yaliyokuwa yakiendelea kupewa kwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamemaliza masomo yao miaka ya nyuma.
Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Ndani kutoka HESLB, Godfrey Sigala alisema bodi hiyo ya mikopo imechukua hatua ya kusitisha mikataba na kampuni za udalali za kukusanya madai ya mikopo na kwamba, kampuni hizo zinatarajiwa kuchukuliwa hatua za kisheria zaidi.
Sigala alisema kuwa hivi karibuni watatoa orodha ya wadhamini wa wadaiwa sugu wa bodi hiyo na kwamba, hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa kwao.
No comments:
Post a Comment