Wednesday, 10 August 2016
MATABIBU WANNE WAKIMBILIA KORTINI
NA FURAHA OMARY
MATABIBU wanne wa tiba mbadala na tiba asili, wamewasilisha maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, wakiomba kuruhusiwa kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa usajili na kusimamishwa kutoa huduma hizo.
Matabibu hao waliowasilisha maombi hayo ni Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium, Abdallah Mandai wa Mandai Herbal Clinic, Tabibu John Lupimo wa Lupimo Suntarium Herbal Clinic na Simon Rusigwa wa Sigwa Herbal Clinic.
Kupitia wakili wao, Dk. Lucas Kamanija, matabibu hao waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo dhidi ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana, mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi. Hata hivyo, upande wa jamhuri uliwasilisha pingamizi la awali kupinga maombi hayo.
Kutokana na kuwasilishwa kwa pingamizi hilo, Jaji Munisi aliamuru kuanza kusikilizwa kwa pingamizi hilo kesho saa nane mchana.
Wakili Dk. Kamanija amewasilisha maombi hayo kwa sababu wanaamini taratibu za kuwafutia wateja wao usajili hazikufuata sheria.
Aidha, wanaamini hawakufutiwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, bali Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambaye kisheria hapaswi kufanya hivyo.
Pia, alidai wanaamini huo wanaosema ni uamuzi si uamuzi bali ni tuhuma mpya, ambazo wateja wao hawakusikilizwa na Kamati ya Maadili ya Baraza hilo na uamuzi huo ulitolewa bila kupitia katika kamati hiyo.
Katika pingamizi la jamhuri, wanapinga maombi hayo kwa madai waombaji hawajapitia njia zote zinazotakiwa kabla ya kufika mahakamani.
Sababu nyingine ya pingamizi hilo la awali ni kwamba hati za viapo hazipo sahihi.
Matabibu hao waliamua kuwasilisha maombi hayo mahakamani baada ya baraza hilo kutangaza kuwafutia usajili Matabibu Kabujanja na Mandai huku matabibu Lupimo na Rusigwa wakisimamishwa kwa miezi sita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment