Wednesday, 10 August 2016

MSAKO WA WAHAMIAJI HARAMU KWA WAANDISHI WA HABARI WAANZA


IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, imetangaza kuanza kwa msako wa wahamiaji haramu kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi hapa nchini kinyume cha sheria.

Aidha,  imewataka waandishi wa habari wenye taarifa za kuwepo  kwa waandishi wa habari wenzao, ambao wanaishi nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria, kupeleka majina katika idara hiyo ili waweze kuchukuliwa hatua  haraka.

Kamishna wa Idara hiyo mkoani hapa, John Msumule, alisema jana kuwa, tayari wameanza kufuatilia na kuchunguza  baadhi ya waandishi wa habari na watangazaji wa kigeni, hususan ambao hawana vibali vya kuishi nchini na kufanya kazi hiyo.

Msumule alisema ni hatari kwa taifa kuwa na waandishi wa habari wa kigeni, ambao wanaishi  kinyume cha sheria, jambo linaloweza kuwafanya kuandika habari za uchochezi na za kuhatarisha usalama,  hivyo ni lazima wachunguzwe na kuchukulia wahatua.

“Tunawataka waandishi wa habari kama itawezekana kote nchini, kuanza kuwaorodhesha waandishi wa habari wenzao wa kigeni, ambao hawana vibali vya kuishi nchini au kufanya kazi hiyo. Hawa waandishi ni hatari na wanaweza kuhatarisha usalama wa taifa letu kwa kutumia kalamu zao. Isitoshe wanaweza kutumia  taaluma hiyo kuingia katika maeneo nyeti na kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu taifa letu,”alionya Msumule.

Alisema waandishi wa habari na watangazaji wa kigeni licha ya kuhatarisha usalama wa taifa kwa kujiingiza katika vyombo muhimu vya habari na wanaofanya kazi hiyo kinyume cha sheria, kunawanyima fursa waandishi wazawa.

“Uandishi wa habari ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Hii ni fursa ambayo waandishi wa hapa nchini wanaweza kuifanya. Natoa wito kwa waandishi wa habari, kama wanaamini katika vyumba vyao vya habari kuna waandishi wanaofanya kazi hiyo  kinyume cha sheria, watupatie taarifa tuweze kuwakamata,”alibainisha.

Alisema tayari msako umeanza ndani ya tasnia hiyo, hivyo kuwataka waandishi wa habari wenyewe kutoa ushirikiano kwa idara hiyo.

No comments:

Post a Comment