Monday, 29 May 2017

SIRRO AAPISHWA KUWA IGP MPYA








Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa za wahalifu waliopo katika maeneo yao jambo ambalo litapunguza au kuondoa kabisa uhalifu nchini.

IGP Sirro ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi la Tanzania.

Amesema kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao hivyo ni wajibu wa jeshi hilo kuhakikisha nchi nzima ina ulinzi wa kutosha utakaopelekea wananchi kuishi kwa amani na utulivu na kuwawezesha kufanya kazi zao bila kubugudhiwa.

“Uhalifu hauwezi kupungua kwa kutegemea Jeshi la Polisi pekee bali tunahitaji nguvu ya pamoja ili kushinda vita hiyo, ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi kikubwa”,Alisema IGP Sirro.

Ameongeza kuwa kipaumbele cha kwanza katika utendaji wake kwenye  nafasi hiyo ni kupambana na uhalifu pamoja nidhamu ya watendaji kazi kwani bila nidhamu, kazi ya kupambana na wahalifu haiwezi kufanikiwa.

Aidha, amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao umekuwa na mauaji na uhalifu wa mara kwa mara kuwa atafanyia kazi changamoto zinazowakabili na  kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu.

Kwa upande mwingine, IGP Sirro amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumuamini na kumteua katika cheo hicho pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda kwa ushirikiano wake wakati alipokuwa akitumikia cheo cha Kamishna wa Polisi wa Kanda maalum ya Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi huo, IGP Sirro alishika nyadhifa mbali mbali zikiwemo za Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamanda wa kikosi cha operesheni maalum na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam.   

No comments:

Post a Comment