Tuesday, 30 May 2017

WABUNGE WA UPINZANI WASHAMBULIWA BUNGENI

WATANZANIA wametakiwa kupuuza kauli za wabunge wa kambi ya upinzani wanazotoa bungeni, kukosoa hatua ya Rais Dk. John Magufuli, kuchukua hatua stahiki katika sakata la mchanga wa dhahabu (makinikia).

Wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2017/2018, bungeni jana, wabunge walisema hatua anazochukua Rais Magufuli ni sahihi na anapaswa kuungwa mkono.

Kauli za wabunge hao zimekuja siku chache baada ya Rais Dk. Magufuli, kupokea taarifa ya kamati maalumu, aliyoiunda kuchunguza mchanga uliokuwemo kwenye makontena ya mchanga wa madini, yaliyoko katika maeneo mbalimbali.

Kufuatia kamati hiyo kubaini wizi mkubwa wa madini, kutokana na mchanga huo kusafirishwa kwenda nje ya nchi kuchenjuliwa, Rais Dk. Magufuli, alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Pia, alivunja Bodi ya TMAA na kumsimamisha kazi mkurugenzi wake.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Shonza, alisema Rais Magufuli, anatakiwa kuungwa mkono baada ya kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na sakata la mchanga wa dhahabu.

Shonza alimshambulia vikali Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (Singida Mashariki-CHADEMA), kwa kauli yake ya kukosoa uamuzi wa Rais Dk. Magufuli kuhusu sakata hilo.

Alisema Rais Magufuli amefanyakazi nzuri na uamuzi wake umepongezwa na Watanzania wanaomtakia mema katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo.

Shonza alisema wabunge wa upinzani wana ajenda ya siri kuhusu utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano.

Alisema wabunge wa upinzani wamezoea wizi na amemuomba Rais Magufuli, kuendelea kuchukua hatua stahiki kwa watendaji wabovu.

Alisema wabunge hao wamekuwa wakipinga mafanikio ya Rais Dk. Magufuli bila sababu za msingi na alitoa mfano wa Lissu.

Mbunge huyo alisema Lissu ni kigeugeu na amekuwa akitoa kauli zenye utata kuhusu serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na ya sasa chini ya Rais Dk. Magufuli.

Alisema awali, wabunge wa upinzani waliiponda serikali ya awamu ya nne kwa madai kuwa ni dhaifu, lakini baada ya Rais Dk. Magufuli kuchukua hatua, wameanza kulalamika.

"Namshangaa Lissu, alikuwa akimponda sana Lowassa (Edward), akidai ni fisadi, leo anazungumza nchi nzima kumnadi ni mtu safi. Rais endelea kuchapa kazi, hawa tumewazoea, kila kitu kwao ni kupinga," alisema Shonza.

Alisema kitendo cha Lissu kumtetea Lowassa, kinathibitisha kuwa wabunge wa upinzani wanakumbatia mafisadi na amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Magufuli.

Kwa upande wake, mbungeCosato Chumi (Mafinga Mjini-CCM), alisema wabunge wa upinzani hawana sababu ya kubeza uamuzi wa Rais Dk. Magufuli, kwa kuwa suala hilo liko wazi kwa kila Mtanzania.

Alisema wabunge waache siasa katika masuala muhimu ya kitaifa na amewataka wapinzani kumpongeza Rais kwa uamuzi wa kuchukua hatua dhidi ya wabadhirifu.

"Jamani ifike wakati tuache siasa. Rais Magufuli anatakiwa kuungwa mkono, tuache kuponda kila kitu. Sakata hili la mchanga wa dhahabu liko wazi na hatua zimechukuliwa, sioni sababu ya kubeza," alisema Chumi.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeomba kuidhinishiwa sh. 150,845,419,000. Kati ya fedha hizo, sh. 142,845,419,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,000,000,000 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment