Tuesday, 30 May 2017

UMOJA WA MATAIFA WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI



UMOJA wa Mataifa umepongeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli, katika kutekeleza vyema kanuni za utalawa bora ndani na nje ya nchi.

Pia, umoja huo umeipongeza Tanzania kwa kudumisha amani barani Afrika, hususan katika nchi za Ukanda wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini kwa Afrika.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, alipowasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2017-2018.

Balozi Mahiga alisema, pongezi hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alipowasili nchini Machi 9, mwaka huu, akiwa njiani kwenda New York, Marekani.

Alisema katibu mkuu huyo alitoa kauli hiyo, alipofanya naye mazungumzo kwa muda mfupi, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akimwakilisha Rais Dk. Magufuli, katika mazungumzo hayo.

"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk. John Magufuli, kwa uwezo wake wa kutekeleza kanuni za utawala bora ndani na nje ya nchi," alisema Balozi Mahiga.

Waziri huyo alisema Guterres pia, alipongeza jitihada za Rais Dk. Magufuli katika kutatua migogoro ya kisiasa katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Alisema Tanzania ilishiriki kikamilifu katika kutatua migogoro ya kisiasa, ambapo Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Rais Dk. Magufuli, walikuwa mstari wa mbele kurejesha amani katika nchi hizo.

Aidha, Balozi Mahiga alisema, serikali itaendelea kudumisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa, mashirika ya fedha na mataifa mengine yanayolenga kuboresha huduma za kijamii.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa na mashirika mbalimbali, walitembelea Tanzania, ambapo walijadiliana namna ya kuisaidia nchi kuendeleza na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta za afya, mazingira na uhamiaji.

Balozi Mahiga alisema, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, liliipatia Tanzania msaada wenye thamani ya Dola za Marekani 831,000, uliojumuisha magari manne ya wagonjwa na mawili ya huduma na vifaa tiba.

Waziri huyo pia alisema kuwa, uhusiano baina ya Tanzania na Israel umeimarika baada ya nchi hiyo kutoa msaada wa kufadhili mafunzo ya tiba ya moyo kwa madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Alisema hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa Tanzania, kwa kuwa itapunguza gharama za kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi.

"Serikali ya Israel imetoa msaada wa mchoro wa kituo cha maafa kinachotegemewa kujengwa eneo la Msalato, Dodoma. Pia, wataalamu kutoka Israel, wanategemewa kuja nchini Juni, mwaka huu, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, utakaowezesha kuchora mchoro huo," alisema Balozi Mahiga.

Waziri huyo alidokeza kuwa, ujenzi wa kituo hicho cha kimataifa utaongeza uwezo wa Dodoma, kukabiliana na maafa, ikizingatiwa kuwa, mkoa huo unatarajiwa kupokea wageni wengi kutokana na azma ya serikali kuhamia Dodoma.

Alisema kwa mara ya kwanza tangu taifa lipate Uhuru, Tanzania inafungua ubalozi katika mji wa Tel Aviv, mwaka huu na itapata manufaa katika kupata utaalamu wa kilimo cha ugwagiliaji, TEHAMA, ulinzi na utalii.

No comments:

Post a Comment