Sunday, 11 June 2017

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA UCHUNGUZI WA SALFA


*Ni ya makontena 211 yaliyokuwa bandarini Dar
*Yabainika kuwa inafaa kwa matumizi ya kilimo
*Asisitiza wakulima waanze kupulizia mikorosho

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema salfa iliyoingizwa nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa matumizi ya kupulizia kwenye mikorosho.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 10, 2017) wakati akizungumza na wajumbe wa kamati maalum, waagizaji wa salfa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Korosho nchini (CBT) kwenye kikao alichokiitisha kwenye makazi yake, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
“Bodi kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili waanze kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu umeshaanza,” amesema.
Juni 4, mwaka huu Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa ulioko bandari ya Dar es Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI kuwa ya salfa iliyoingizwa nchini na kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba ya Bodi ya Korosho haijakidhi viwango.
Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna mkanganyiko miongoni mwa wakulima juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya kuwa Serikali ilikwishapokea taarifa ya bodi, na taarifa ya kampuni iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa taarifa ya uchunguzi wao mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele alisema walifanya uchunguzi kwenye makontena 21 ambayo ni sawa na asilimia 10 ya makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity na moisture contentskama ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa kutoka GALCO Inland Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa salfa ulioletwa na kampuni ya ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema.
“Kwa kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanyika, viwango (specifications) vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango vya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha salfa ni maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha (containers) 211 unakidhi viwango,” alisema kwenye taarifa yake.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Maokola Majogo alisema yeye pamoja na Bodi yake watatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu na akawataka wakulima wasisite kutumia salfa hiyo kwani imekwishathibitishwa na Mkemia Mkuu kwamba haina matatizo.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Hassan Jarufu alisema Bodi iliagiza salfa kwa kiwango kile kile cha mwaka jana kilichotumiwa na wakulima na kuleta matokeo mazuri.
“TPRI walichukua sampuli na kuleta majibu kuwa ina mapungufu, kwa hiyo tukashindwa kuisambaza. Mheshimiwa Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu afanye uchunguzi wake, na sisi tumefurahia matokeo na tunaenda kutekeleza maelekezo yake ya kututaka tusambaze salfa kwa wakulima,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JUNI 10, 2017.

No comments:

Post a Comment