Saturday 29 August 2015

LOWASSA APANIA KUVUNJA REKODI YA MAGUFULI, MELI ZAKODIWA KULETA WANAWAKE DAR KUTOKA Z'BAR



NA WAANDISHI WETU

KATIKA kile kinachoweza kuitwa usanii wa aina yake, CHADEMA ambayo leo inazindua kampeni zake za urais, imeamua kukodi meli mbili kusafirisha wanawake kutoka Zanzibar kwa ajili ya mkutano wao huku wakiwa wamepanga kupambana wavunje rekodi ya CCM.

Mkutano huo ambao unatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Jangawani, Dar es Salaam, unatarajiwa kupambwa na kinamama hao watakaokuwa sehemu ya wafuasi wao.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili lilizipata jana, kutoka miongoni mwa vyama washirika wa UKAWA zilisema wamedhamiria kuvunja rekodi zote zilizowekwa wiki moja iliyopita wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwenye mkutano wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alisema idadi ya watu waliohudhuria mkutano ule ilikuwa  kubwa kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Mmoja wa viongozi wa UKAWA aliliambia gazeti hili wanakusudia kuvunja rekodi hiyo.

“Kama CCM walipata watu wengi, sisi tutakuwa na watu zaidi ya hao. Magufuli alizungumza kwa dakika 53 sisi tunataka Lowassa azungumze kwa muda mrefu zaidi. Tumemuandalia hotuba itakayotumia muda wa saa 1:18 (saa moja na dakika kumi na nane),” alisema kiongozi huyo kutoka mkoani Arusha.

Hata hivyo, gazeti hili linao uhakika kwamba Lowassa hana ubavu wa kuzungumza muda mrefu jukwaani, na kwamba, pia hawezi kushika vipaza sauti vingi kwa wakati mmoja kwa muda mwingi huku anazungumza.

Tangu ajiunge na Chadema mwishoni mwa mwezi uliopita, Lowassa amekuwa akitumia muda mfupi kuhutubia, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wamelihusisha na hali yake ya kiafya.

Habari zaidi kutoka ndani ya vyama hivyo zilikariri kuwepo kwa meli mbili za kukodi zilizosheheni wanawake kutoka Zanzibar zinazowasili kuongeza idadi ya watakaohudhuria.

Habari hizo zinakuja huku baadhi ya wafuasi kama hao kutoka mikoa tofauti nchini hususan Arusha na Kilimanjaro, wakimiminika Dar es Salaam kutimiza azma hiyo, huku wanaotoka Zanzibar, wakilengwa kuonyesha picha ya umoja wa kitaifa.

Kuwasili kwa kinamama hao wanaolengwa kutimiza azma hiyo ya kisiasa kumezua maswali kutoka kwa wakazi wa Visiwani juu ya namna ya utekelezaji wake unahofiwa kukiuka maadili yanayoheshimiwa na Wazanzibar ambapo wanawake na wanaume hawachanganyiki pamoja.

Hadi jana jioni gazeti hili linaenda mtamboni, halikuweza kubaini hasa kama kuna utaratibu maalumu ulioundwa kukidhi matakwa ya utamaduni huo wa Zanzibar.

Imebainika kigezo cha UKAWA kukusanya wafuasi kutoka sehemu tofauti za nchi ni kuongeza idadi ya wahudhuriaji wakijirabu kupiku rekodi iliyowekwa kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea wa CCM, Jumapili iliyopita katika viwanja hivyo ambavyo 'viliotapika’ na pia waonekane wana ushiriki wa kitaifa

No comments:

Post a Comment