Saturday 29 August 2015

SAMIA AACHA GUMZO KARATU, MBULU, BABATI



NA EPSON LUHWAGO, BABATI

MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, jana aliteka miji ya Karatu, Mbulu na Babati katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Samia, katika mikutano yote aliyoifanya jana, kulikuwa na umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wakikongwa nyoyo zao kutokana na ahadi kemkem alizokuwa akizitoa.

Kuwepo kwa wingi huo wa watu kumeanza kurejesha imani kwamba majimbo ya Karatu na Mbulu ambayo yalikuwa chini ya CHADEMA miaka mitano iliyopita.

Hali hiyo ilijitokeza katika maeneo ya Kambi ya Simba na Endabash (Karatu), Mbulu Mjini, Magara na Magugu (Babati Vijijini) na Babati Mjini.

Katika jimbo la Karatu, mikutano aliyoifanya ilikuwa na watu wengi tofauti na ilivyokuwa ikidhaniwa kutokana na jimbo hilo kuwa chini ya CHADEMA kwa miaka 20, tangu mwaka 1995.

Wananchi waliojitokeza katika mikutano hiyo, walionyesha wazi kwamba CCM ina nafasi ya kurejesha jimbo hilo katika himaya yake baada ya kulipoteza katika kipindi hicho.

Katika mkutano mwingine alioufanya kwenye Uwanja wa Mpira Mbulu Mjini, alipata mapokezi makubwa hali ambayo pia ilirejesha matumaini kuwa CCM itashinda katika majimbo ya Mbulu Mjini na Mbulu Vijijini.

Hali kama hiyo iliyoonyesha kuwa CCM itaibuka na ushindi wa kishindo wakati msafara wake ukitoka Mbulu kwenda Babati ambapo wananchi waliuzuia mara tatu.

Safari ya kwanza ilikuwa kwenye kijiji cha Magara, jimbo la Babati Vijijini ambapo baada ya kuingia wilayani humo, alikutana na ‘mafuriko’ ya watu ambao walisimamisha msafara wake. Baada ya kuwahutubia waliridhika na kutoa nafasi ya kuendelea na safari.

Msafara huo ulizuiwa pia katika vijiji vya Mbuyu wa Mjerumani na Magugu jimbo la Babati Vijijini ambapo wananchi walifunga barabara na kumfanya awahutubie.

AHADI ZAWAKONGA NYOYO

Katika mikutano yote hiyo, wananchi walionekana kukongwa na ahadi alizokuwa akizitoa, kwani walikuwa ‘wakipagawa’ na furaha huku wakishangilia kila mara.

Miongoni mwa ahadi alizozitoa ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami zikiwemo za Mbulu hadi Karatu na Mbulu hadi Mbuyu wa Mjerumani, wilayani Babati kwa kiwango cha lami.

Alisema barabara hizo zitajengwa katika miaka mitano ijayo ya Serikali ya CCM kwa kuwa ziko katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema barabara hizo zitachochea ukuaji wa uchumi na kuwaondolea wananchi adha ya usafiri.

Kuhusu huduma za afya, alisema serikali ijayo itahakikisha dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya zinapatikana kwa wingi na kupambana na watumishi wote wanaojihusisha na wizi.

“Haiwezekani mtu aende hospitalini na kuambiwa hakuna dawa na wakati huo huo anaambiwa aende kwenye duka fulani la dawa.

 Amejuaje kuwa dawa ziko kwenye duka hilo? Watu kama hawa hatutakuwa na msalia mtume nao hata kidogo,” alisema katika mikutano hiyo.

Kwa upande wa migogoro ya ardhi, alisema kazi kubwa itakuwa kupima ardhi na kutenga kwa ajili ya wakulima na wafugaji na pia kurejesha mashamba ambayo yalichukuliwa na wawekezaji bila kuendelezwa.

Naye Mjumbe wa Kampeni ya CCM Kitaifa, Christopher ole Sendeka, aliwalipua mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, kuwa ni wasaliti na wanapaswa kuogopwa kama ukoma.

Sambamba na hilo, amesema Watanzania wanapaswa kuichagua CCM na kuitosa CHADEMA na umoja wao wa UKAWA kwa kuwa vyama hivyo vimenunuliwa na Lowassa kama bidhaa ya dukani au sokoni.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni mjini Babati, Ole Sendeka alisema Lowassa alienguliwa kuwa mgombea urais kutokana na kukosa vigezo kwa mujibu wa Katiba, miiko na maadili ya Chama.

Kwa upande wa Sumaye, alisema amejivunjia heshima ndani ya jamii kutokana na kuwa kigeugeu hali iliyomfanya ashindwe kuaminika tena kwa Watanzania.

“Miezi minne iliyopita nikiwa katika Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tulikwenda nje ya nchi na balozi mmoja alituuliza tunadhani ni nani anaweza kuwa Rais wa Tanzania.

“Binafsi nilisema sijui na alipouliza Lowassa je, nilisema huyo hawezi kwa sababu hana sifa kwa sababu hana vigezo kutokana na kukiuka maadili, kanuni na viapo vya uanachama wa CCM.

“Katika Katiba ya CCM kuna ahadi za mwanachama kuhusu rushwa na cheo ambapo mwanachama yeyote anakatazwa kutokujihusisha na vitendo vya rushwa na pia kutumia cheo kwa manufaa binafsi.

Lowassa alishakiuka ahadi hizo hivyo hakustahili kuwa Rais wa Tanzania kupitia CCM.

“Kwa mantiki hiyo, binafsi nilishampima na kumwona kuwa hawezi kuwa Rais na CCM ingefanya kosa kubwa kumpitisha kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa mwaka huu. Hata sasa hafai kuwa Rais na Watanzania tunapaswa kulijua hilo,” alisema.

Kuhusu Sumaye, alisema ameonyesha uhalisia wake kutokana na kuwa kigeugeu kwa kula ‘matapishi’ yake kutokana na kauli tata alizozitoa juu ya Lowassa.

“Kaka yangu Sumaye alisema iwapo CCM ingempitisha Lowassa kuwa mgombea urais, angejitoa katika Chama. Alipoulizwa ni kwa nini alisema ni mtu fisadi na asiye na maadili.

"Lakini cha ajabu siku chache zilizopita ameungana naye,” alisema na kuongeza kuwa ukigeugeu huo umemfanya thamani yake ishuke ndani ya jamii ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment