Sunday 30 August 2015

TUTAJENGA HOSPITALI YA RUFANI SINGIDA-SAMIA

 Umati wa wananchi ukimsikiliza Mgombea Mwenza kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu alipohutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Msange, Singida Kaskazini
 Umati wa wananchi ukimsikiliza Mgombea Mwenza kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu alipohutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Msange, Singida Kaskazini
Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan akiwasalimiabaadhi ya viongozi, baada ya kuwasili  katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika jimbo hilo.
 Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan akimnadi Mgombea Ubunge Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, katika mkutano uliofanyika katika jimbo hilo
 Mgombea Ubunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba akiselebuka na baadhi ya viongozi na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo, katika eneo la Kyengege, Iramba mkoani Singida,



NA EPSON LUHWAGO, SINGIDA

HOSPITALI kubwa ya kisasa inatarajiwa kujengwa mkoani hapa, ambayo itakuwa ya rufani kwa mkoa wa Singida na mikoa inayouzunguka, imeelezwa.

Hayo yalisemwa jana na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa katika mikutano  ya kampeni ya Chama Singida Mjini na Kyengeja, wilayani Iramba.

Samia alisema hospitali hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa na itahudumia wagonjwa kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Tabora, Simiyu na Manyara.

“Hospitali hii itakuwa ya rufani kama ile ya Muhimbili (Dar es Salaam) na itapunguza adha ya kufuata huduma Dar es Salaam au Mwanza. Kukamilika kwa hospitali hii kutawezesha huduma bora za afya kupatikana kwa urahisi,”alisema.

Sambamba na hospitali hiyo, alisema huduma za afya zitaboreshwa zaidi kwa kuongeza wataalamu na vifaa tiba.

Mbali na huduma za afya, alisema mkazo mkubwa mwingine utakuwa katika ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao na kuchakata madini ili viweze kutoa ajira kwa vijana na wananchi wa mkoa wa Singida.

Miongoni mwa viwanda hivyo, kwa mujibu wa Samia, ni vya kusindika mafuta ya alizeti kutokana na mkoa huo kuzalisha zao hilo kwa wingi kulinganisha na mikoa mingine.

Alisema kwa sasa kuna viwanda vidogo vya kutengeneza mafuta hayo lakini kuna kiwanda kikubwa ambacho kinajengwa katika eneo la Ndago.

Samia alisema kukamilika kwa kiwanda hicho kutawezesha kutoa ajira zaidi kwa vijana hivyo kupunguza tatizo hilo ambalo ni kubwa nchini kote.

“Kiwanda hiki kikikamilika kitachuja mafuta kwa mara ya pili (double refinery) ambayo yatakuwa na ubora wa hali ya juu yatakayoweza kuuzwa katika masoko ya kimataifa,” alisema.

Samia alisisitiza kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho na vingine ambavyo viko mkoani Singida vitaweza kuajiri zaidi ya vijana 600.

Mgombea mwenza huyo alisema serikali ijayo ya CCM itahakikisha inasambaza umeme kwa kasi zaidi kwenye vijiji.

Kwa mujibu wa Samia, umeme huo utachochea ukuaji wa uchumi kwa kuwa wananchi wataweza kuanzisha viwanda vidogo vya kutengeneza vitu mbalimbali.

Katika mkutano wake wa kwanza mkoani Singida katika kijiji cha Msange, Jimbo la Singida Kaskazini, alisema tatizo la maji ambalo linavikabili vijiji vingine vya Singida, litapatiwa ufumbuzi katika serikali ijayo ya awamu ya tano chini ya CCM.

Pia alisema elimu alisema jitihada kubwa zitakuwa ujenzi wa mabweni na kukamilisha maabara ili kuwezesha watoto wengi hususan wa kike, kutoendelea kukatisha masomo kutokana na mimba.

“Kujengwa kwa mabweni haya, kutawezesha watoto wengi kukaa shuleni kwani watakuwa katika mazingira rafiki tofauti na sasa ambapo wanatembea umbali mrefu kuwenda shuleni na kurudi nyumbani,” alisema.

NYALANDU NA HELIKOPTA

Mgombea Ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandi, jana aliteka hisia wa wananchi waliokuwa kwenye mikutano ya kampeni za CCM pale alipotua kwa helikopta.

Nyalandu ambaye anagombea kwa mara ya nne katika jimbo hilo, aliwasili kwa ‘chopa’ hiyo saa 4.57 katika kijiji cha Msange ambapo baada ya kutua mkutano ulilipuka furaha huku Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, akihanikiza kuwa ‘jembe linaingia’.

Mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alitua kwa usafiri huo katika mikutano iliyofanyika Kyengege jimbo la Iramba na Singinda Mjini ambako mkutano mkubwa ulifanyika kwenye viwanja vya CCM Mkoa.

Kutumika kwa usafiri huo na kiongozi huyo, kulikuwa kinogesho cha aina yake kwa kuwa alikuwa akitua baada ya watu kukusanyika na wakati mwingine kuanza kwa shughuli za kampeni sehemu husika.

MWIGULU ATOA NENO

Naye Mwigulu Nchemba, anayetetea kiti cha ubunge Jimbo la Iramba, alisema mambo ambayo CCM imeyafanya katika mikoa wa Singida, ni mtaji tosha kwa Chama kushinda tena kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Alisema CCM imefanya mambo makubwa kwa kujenga shule za sekondari katika kila kata na kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi za vijiji kwa kujenga zahanati.

Kwa mujibu wa Mwigulu, hata ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ni ishara tosha kuwa CCM inataka kurejea ili kuwaleta wananchi maendeleo zaidi.

“Hivi sasa katika jimbo la Iramba kwa mfano, kuna umeme katika vijiji vingine na kazi ya kupeleka kule ambako haujafika inaendelea.
Tunahitaji kuichagua tena CCM ili kumalizia kazi hii,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Yule ambaye atawapigia wapinzani atakuwa anapoteza muda na nguvu zake. CCM itashinda na kuendelea kushika dola. Wapinzani hao hawana uwezo kwasababu ni waigizaji na kuishindanisha CCM na waigizaji ni jambo ambalo haliwezekani.”

Mwigulu, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, aliwataka wananchi waliojitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu, ili waichague CCM na kuipa ushindi wa kishindo.

No comments:

Post a Comment