Sunday 13 September 2015

ASKOFU GWAJIMA ANA AKILI MBILI?




Na Omar Mohammed
NILIKUWAPO kwenye ukumbi wa hoteli ya Landmark, Ubungo, Dar es Salaam, siku Josephat Gwajima, anayejiita kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alipokutana na waandishi wa habari, Septemba 8.
Ulikuwa ni mkutano wa Gwajima na waandishi wa habari, mkutano ambao hata hivyo haukuwa na tofauti yoyote na kanisani kwake, kutokana na kufurika kwa waumini wake, kiasi cha watu kukosa hewa na kupumua kwa shida kwa sababu ya wingi wa watu.
Kwa hakika kabisa, kikubwa nilichokiona ndani ya akili na moyo wa Gwajima baada ya mkutano ule aliouitisha kwa madai ya kutaka kujibu tuhuma za rushwa ya fedha kutoka kwa Edward Lowassa zilizoelekezwa kwake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, ni kuwa na akili mbili.
Katika tuhuma hizo, Gwajima anadaiwa kusambaza kwa njia ya ndege fedha za rushwa kutoka kwa Lowassa kwenda kwa maaskofu wa makanisa mbalimbali nchini, wakiwamo wa Kanisa Katoliki kwa lengo la kushawishi viongozi hao wa dini wamuunge mkono katika mbio zake za urais.
Baada ya kumtazama kwa macho yangu na kumsikiliza Gwajima kwa masikio yangu, nilihitimisha nikiwa na wazo moja tu, la kwamba huyo anayejiita kiongozi wa kiroho, ana akili mbili!
Kwanini? Nilivyomwona Gwajima wakati wote wa zaidi ya saa moja alizozungumza katika mkutano ule, kuna wakati alizungumza vitu vyenye akili, akionekana kuwa mzalendo wa kweli kwa Taifa lake hili, lakini kuna wakati alionekana kama akili zake zimefyatuka!
Gwajima ana akili mbili. Akili ya kwanza inaonesha kwamba Gwajima ana uzalendo wa kweli na anathamini amani, umoja na mshikamano katika Taifa letu hili viendelee kuwepo, na kwa hiyo hayuko tayari kuona mtu yeyote akizichezea tunu hizo kuu za Taifa la Tanzania.
Lakini Gwajima huyo huyo ana akili nyingine ya pili inayomwonesha kwamba yeye ni wakala namba moja wa maadui wa nchi hii wa ndani na nje, wenye nia na dhamira ovu ya kuvuruga amani, umoja na mshikamano wa Taifa hili.
Wakati Gwajima anaanza mkutano, mwongozaji ambaye pia ni Mchungaji kama alivyo yeye, katika utangulizi wake kabla ya kumkaribisha kiongozi huyo anayejiita wa kiroho, alielezea kuhusu umuhimu wa kulinda mbegu ya amani, umoja na mshikamano wa Taifa hili.
Mchungaji huyo, alisema mbegu hiyo ya amani iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere haina budi kulindwa na kila Mtanzania kwa nguvu zake, ili kuhakikisha hakuna mtu, kiongozi wala mwanasiasa anayeichezea.
Baada ya Mchungaji huyo kumkaribisha Gwajima ili atoe yaliyokuwa moyoni mwake, nilimtarajia kuyakana kwanza maneno ya Mchungaji wa Kanisa lake, lakini hakufanya hivyo, ikiwa ni ishara na dalili, kwamba kiongozi huyo, alibariki maneno yale na kukubaliana na Mchungaji yule.
Tukio la pili, Gwajima akiwa katikati ya mazungumzo yake, alitamka kwamba Kanisa Katoliki, ndilo Kanisa Kuu kwa makanisa yote nchini na kwamba mapadri na maaskofu wake wanapaswa kuheshimiwa na kila mtu mwenye imani na mfuasi wa Yesu Kristo!
Maeneo haya mawili. Umuhimu wa kila Mtanzania kuilinda na kuienzi mbegu ya amani, umoja na mshikamano vilivyojengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na ukuu wa Kanisa Katoliki, yalitokana na akili halisi ya Gwajima.
Kwa nini akili halisi ya Gwajima? Kila mmoja anakumbuka jinsi kiongozi huyo wa kiroho alivyomtusi, kumkejeli na kumdhalilisha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo pamoja na Kanisa lake la Kikatoliki, mbele ya waumini wake, lakini huyo huyo, katika mkutano wake huo wa wiki hii, aligeuka maneno yake na kuwapa ukuu wa kutukuka mapadri na maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa lao.
Hadi sasa, kutokana na matusi hayo, kejeli hizo na udhalilishaji huo dhidi ya Askofu Pengo na Kanisa Katoliki, Gwajima anakabiliwa na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa kuwa suala hili la Pengo na Gwajima liko mahakamani, basi tuliachie hapo. Itoshe tu kusema kwamba haiwezekani Gwajima huyo huyo, aliyemdhalilisha Askofu Pengo ndani ya Kanisa lake akidai kwamba amekula na kuvimbiwa maharage, leo hii ageuke na kutangaza ukuu na utukufu wa mapadri, maaskofu na Kanisa Katoliki!
Lakini Gwajima huyu huyu, katika akili yake ya pili, yeye haoni hatari kwa matajiri wenye fedha zao, mafisadi waliofisidi rasilimali za nchi hii hata kabla hawajakamata nchi, wakamate Dola ili kukomba kila rasilimali ya nchi kwa manufaa yao, familia na ndugu zao.
Gwajima anasema wakati wa mafisadi kushika hatamu za uongozi wa nchi hii ni sasa, hata watu wafanyeje, hakuna wa kuwazuia na yeye yuko mstari wa mbele kuwasaidia na kuwapigania wakamate Dola.
Gwajima anakwenda mbali zaidi kiasi cha kumkufuru hata Mwenyezi Mungu. Katika mkutano huo, alisema Yesu Kristo alipata misukosuko mingi kutoka kwa watawala na watu wa enzi zake, kiasi cha kumkamata na kumuua kwa kumsulubu msalabani, lakini hatimaye aliwashinda wote baada ya kufufuka na hadi leo bado anaitawala dunia.
Katika hilo la Yesu, Gwajima alitolea mfano mwingine wa Mtume Muhammad (S.A.W) pia kwamba alipata misukosuko mingi kutoka kwa watu wa enzi zake, waliokuwa wakimzuia na kumpinga asieneze ujumbe wa Mwenyezi Mungu, lakini Mtume aliwashinda na hadi sasa jina la Mtume linaendelea kuitawala dunia.
Kwa hiyo, kwa mifano hiyo miwili ya Yesu na Mtume Muhammad pamoja na mfano wa tatu alioutoa kuhusu Mfalme wa Wabudha kwa wenye imani ya Kibudha, Gwajima anasema hakuna Mtanzania wala nguvu yoyote kwa wakati huu itakayomzuia fisadi kwenda Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ili sasa Ikulu ya Tanzania igeuzwe pango la walanguzi.
Hii ya pili haiwezi kuwa akili ya mtumishi wa Mungu, wala ya kiongozi wa kiroho, bali ya mtu mwenye pepo mbaya, mwenye nia na dhamira ovu ya kutaka kuliangamiza Taifa hili la Tanzania na kizazi chake.
Anachosahau Gwajima ni kwamba Taifa hili, kama alivyosema siku ile Mchungaji mtangulizi wake, mbegu za misingi yake na nguzo zake, zilisimikwa na Mwalimu Nyerere kwa baraka zote za Mwenyezi Mungu!
Kwa hiyo, Mungu aliyelipigania Taifa hili likafukuza wakoloni wa Kiingereza bila kumwaga damu, ataendelea kulilinda na kulipigania hata kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, ili liweze kupata rais anayemtii Mungu kwa kauli na vitendo, rais atakayeienzi na kulinda vyema mbegu iliyopandwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.


No comments:

Post a Comment