Sunday, 13 September 2015
SHAKA AZIDI KUTEMA CHECHE
Na Mwandishi Wetu, Njombe
KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema sera na mikakati ya ujenzi na ufufuaji viwanda na masharika ya umma ikiwemo bandari na kuendelea kuimarisha uwekeza chini ya Rais mpya Dk. John Magufuli wa CCM, kutamazliza kero ya ajira hapa nchini.
Shaka alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Matinganjora Kata ya Ikuna kwenye Halmashauri ya Njombe Vijijini mkoani hapa.
Alisema licha ya ajira kuwa tatizo linaloitatiza Afrika na dunia chini ya sera na mikakati ya Mgombea urais wa CCM Dk. Magufuli, tatizo la ajira hasa kwa vijana litapatiwa ufumbuzi na kubaki historia.
Kwa mujibu wa Shaka, suluhisho la tatizo la ajira limeanishwa na kuwekewa mikakati ya kitaalamu kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020 na kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa huku ikijipanga kufufua na kuviboresha viwanda na mashirika ya umma zikiwemo bandari za Mtwara, Lindi na Tanga.
"Ikijengwa reli mpya, viwanda, kuhuisha viwanda vilivyokufa na masharika ya umma tatizo la ajira kwa vijana wenye elimu ya juu na litasahaulika chini ya serikali ijayo ya Dk. Magufuli," alisema Shaka.
Katibu Mkuu huyo alisema ujenzi wa viwanda vya kusindika matunda, chai, kahawa na vile vya kuchakata samaki vitapunguza tatizo la ajira kama si kumaliza kabisa.
Shaka aliwaeleza wananchi hao kwamba Dk. Magufuli ni kiongozi mwenye dhamira, malengo na anayejua, kuthamini na kuhangaikia shida za wananchi wa Bara na Zanzibar.
Akizungumzia vijana wengi wasomi kukosa ajira na wazee kuendelea kubaki maofisini bila kustaafu, Shaka alisema kwa mujibu wa sheria mtumishi wa umma hutakiwa kustaafu baada ya miaka 60, lakini alisifu na kuipongeza serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kuwainua vijana wengi katika ngazi mbalimbali za utumishi wa umma ikiwemo kuwaamini na kuwateua kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo ya wakuu wa wilaya, mikoa, wakurugenzi, makamishna na makatibu wakuu.
"Rais Kikwete ataondoka madarakani akiwa na heshima ya hali ya juu, amewathamanini mno vijana, amewainua na kuwakabidhi majukumu na nafasi nyeti. Pia hakuwabagua wazee na wanawake katika mihimili yote ya dola," alisema.
Alisema ni kawaida ya serikali ya CCM kutekeleza kwa vitendo ahadi zake hivyo alisema anaamini kukua kwa kasi kwa uchumi, ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na ukusanyaji kodi kwa kiwango cha juu, utaendelezwa na Rais ajae kutoka CCM.
Aidha, Shaka aliwataka wananchi na wakazi wa jimbo la Lupembe kumchagua kwa kishindo Dk. Magufuli na mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Yolam Hongoli na mgombea udiwani Kata ya Ikuna, Valantino Hongoli ifikapo Oktoba 25, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment