Sunday, 13 September 2015

SAMIA; TUTABORESHA HUDUMA ZA AFYA KILA KATA


NA ABDALLAH MWERI, TUNDURU
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itatoa kipaumbele cha kwanza katika kuboresha huduma za afya kwa kila kata nchini.
Samia alitoa ahadi hiyo juzi katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni ambapo alifanya mkutano katika Kata ya Mchoteka, Wilayani Tunduru.
Samia alisema Watanzania wanahitaji afya bora ili wafanye kazi kwa ufanisi na aliwataka kumchagua Dk. John Magufuli kwa kuwa ni kiongozi shupavu, mwadilifu na mchapakazi hodari.
"Serikali ya awamu ya tano ya Dk. Magufuli itazingatia zaidi suala la afya kwa sababu tuna amini afya zikiwa bora, kauli mbiu yetu ya Hapa Kazi Tu itatekelezwa kikamilifu," alisema Samia huku akishangiliwa na umati wa wakazi wa Kata ya Mchoteka.
Samia alisema Dk. Magufuli, ameonesha mfano mzuri wa utendaji kazi katika wizara zote alizowahi kuziongoza ikiwemo Wizara ya Ujenzi anayoiongoza hadi sasa.
Alisema Dk. Magufuli sio mbaguzi na ana uhakika atawatumikia vyema Watanzania kama alivyokuwa akifanya katika wizara zote ambapo alikuwa mtendaji mahiri.
Samia aliahidi kutoa gari la wagonjwa katika Kata ya Mchoteka.
Kuhusu elimu, Samia alisema serikali ya awamu ya tano itaimarisha ujenzi wa mabweni ili kuwakomboa wanafunzi wasichana wasirubuniwe na wanamume wakware.
Mgombea mwenza huyo alisema serikali ya Dk. Magufuli itahakikisha inaongeza ujenzi wa shule za kata kwa kidato cha tano na sita ili kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Aliwataka wakazi wa Kata ya Nalasi kupiga kampeni kwa amani na kutumia vyema fursa hiyo kuipa ridhaa CCM kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema CCM ndio chama sahihi kwa Watanzania na amewataka Watanzania wasifanye kosa kuchagua chama cha upinzani kwa kuwa wanaosaka madaraka hawana jipya.
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Angella Kairuki, alisema mabadiliko yanatakiwa kufanywa kwa vitendo na CCM ndio chama pekee chenye kuwaletea maendeleo Watanzania.
Alisema baadhi ya wagombea wa upinzani wamekuwa wakipanda jukwaani wakidai wakishika dola watafuta Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), badala yake wataanzisha vyuo vya ufundi jambo ambalo si sahihi.
Alisema JKT ipo kwa mujibu wa sheria, serikali ya CCM itahakikisha inaboresha na kuimarisha vyuo vya ufundi ili kuendelea kutoa wataalamu.
Msafara wa mgombea huyo mwenza ulikuwa ukisimamishwa mara kwa mara na wakazi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Namtumbo na Tunduru ambapo alipata fursa ya kuzungumza na kujibu maswali ya wakazi wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment