Sunday, 13 September 2015
WANAOTAKA KULIGAWA TAIFA KWA UDINI, UKABILA WAONYWA
Na Samson Chacha, Tarime
MJUMBE wa Kamati ya Maadili ya CCM, Jeremia Wambura, amewataka wananchi kutowapigia kura wagombea wanaotaka kuligawa taifa kwa misingi ya dini na ukabila.
Wambura alisema CCM imeliongoza taifa katika kipindi cha miaka 50, kwa amani na utulivu na kwamba katika kipindi hicho imefanikiwa kuboresha miundombinu na kuinua kipato cha wananchi pasipo kujali dini wala ukabila.
Wambura alisema hayo, katika mkutano wa kampeni za kuwanadi wagombea ubunge na udiwani pamoja na wilayani Tarime mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM wilaya hiyo, Joh Gimunta, alisema Chama kimewateua wagombea wazuri wenye sifa zilizotukuka.
Alisema mgombea urais wa CCM Dk. John Magufuli ni kiongozi imara na mahiri, hivyo aliwataka wananchi kumchagua ili aweze kuliongoza taifa.
Alisema anaimani kubwa kuwa Dk. Magufuli akiwa rais wa awamu ya tano atafanya mambo mengi ya maendeleo.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuwachagua wabunge na madiwani wa CCM.
Watahadharishwa kwa kuchanganya dini na siasa
TABIA DAFFO, BABATI
VIONGOZI wa dini mkoani Manyara wameonywa kuchanganya dini na siasa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Aidha, wametakiwa kuliombea taifa ili liweze kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi wa madhebu ya dini wilayani Babati.
Alisema viongozi wa dini wamepewa mamlaka makubwa ya kuongoza watu kwa imani zao na kwamba wana jukumu la kuwabadilisha wanaokwenda kinyume na misingi ya dini.
“Amani ikitoweka tutajuta na haitarudi tena sisi ndio wa kwanza kupokea wakimbikizi kutoka nchi za wenzetu waliokosa amani sasa sisi tukikorofisha nani atatupokea,” alihoji.
Bendera alisema viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa na wasikubali kutumika kwa manufaa ya wachache.
Alisema wakati umefika sasa watakaovuruga amani wakemewe kwa nguvu zote.
Bendera aliwataka viongozi hao kuendelea kuwahubiria waumini wao kutenda haki, kuwa wavumilivu na kudumisha upendo miongoni mwao.
Aliwataka kuacha kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa kwani kunaweza kukasababisha mpasuko unaoweza kuliingiza taifa katika machafuko.
Kwa upande wa viongozi wa dini, wamewalalamikia baadhi ya wagombea wanatoa lugha za matusi, kejeli, ukabila na udini.
Walisema iwapo viongozi wa aina hiyo hawatadhibitiwa wanaweza kuwagawa wananchi.
Walivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua kali za kisheria wagombea wanaokiuka maadili ya uchaguzi mkuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment