Sunday 13 September 2015
MUZIKI WA CCM WAMZIDI NGUVU LOWASSA
L Viongozi upinzani wamng'ang'ania kwa kukimbilia kanisani
L Maalim Seif naye atumiwa salamu, atakiwa afunge mdomo
L Wafuasi wa CHADEMA mbaroni kwa kushambulia msafara CCM
L Mgombea urais TLP awapasha UKAWA, unafiki hautawasaidia
Na Happiness Mtweve, Dodoma
KATIKA hali inayoonyesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA ambaye pia ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kuelemewa na kampeni na kutokuwa na kipya cha kuwaeleza Watanzania, juzi, alipata wakati mgumu baada ya wakazi wa Wilaya ya Chamwino kumbana kwa maswali aliyoshinda kuyajibu.
Katika ziara ya kampeni zake mgombea huyo alikuwa katika mkoa wa Dodoma ambapo alifanya ziara katika wilaya mbalimbali ikiwemo Chamwino katika Kijiji cha Mvumi Mission.
Alipofika katika eneo hilo ambapo kama kawaida yake alihutubia kwa dakika 6:14, aliruhusu maswali kutoka kwa wananchi ambao walihoji alivyohusika na suala la Richmond wakimtaka alitolee maelezo.
Pia walitaka awaeleze alivyoshughulikia mapigano ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, ambapo Wamasai walipambana na wakulima na kuwakata mapanga kipindi hicho akiwa Waziri Mkuu.
Aidha walitaka kujua alifanya nini katika sekta ya afya kwenye uongozi wake, na kwa nini hakuwai kwenda Mtera kipindi hicho na anakwenda sasa kuomba kura.
Akijibu maswali hayo, mgombea huyo alisema yote hayo hayana maana na kwamba, atajibu swali la afya ambapo alieleza alijenga vituo vya afya na zahanati.
Katika Wilaya ya Bahi mkoani hapa mgombea huyo alishindwa kupanda ngazi wakati akipanda jukwaani hali iliyomlazimu mlinzi wake akishirikiana na mlinzi wa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, kumsaidia.
Hapo napo alihutubia wananchi waliokusanyika kwa muda wa dakika 2:28 ambapo katika Manispaa ya Dodoma alitumia dakika nane tu zilizoacha maswali mengi ikiwemo namna gani atasimamia majukumu ya serikali ambayo humtaka kiongozi wa nchi wakati mwingine afanye kazi hadi usiku wa manane au kuzungumza na kusimama kwa muda mrefu.
Akihutubia wananchi Wilaya ya Dodoma mjini katika uwanja wa barafu, Lowassa ambaye alipanda jukwaani saa 12:08, alisema wamekuwa na uhusiano mzuri na polisi, hivyo ili asiwaudhi atatumia muda wa dakika tano kuzungumza.
Mgombea huyo alisema atawakumbuka watu wote waliosimama kumtetea na anawahakikishia kushirikiana nao kikamilifu.
Hata hivyo hatua hiyo, Lowassa kutumia muda mfupi kuhutubia wananchi ilionekana kuwakera wafuasi wake ambapo walisikika wakiteta juu ya hali ya afya yake pamoja na namna anavyoendelea kupoteza haiba waliyoizowea ya uchangamfu.
“Jamani kwanini anafanya hivyo, hivi kweli unaweza ukahutubia dakika tano huku watu wana hamu ya kukusikiliza, kama kupumzika mbona amepumzika si wamekuja tangu jana sasa kwa nini bado anatumia muda mfupi,” alisikika mmoja wa wafuasi hao akizungumza na mwenzake.
Kutoka Pemba mwandishi Masanja Mabula, anaripoti kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid Mohammed, amewataka wananchi kuwaepuka viongozi wanaotumia nyumba za ibada kuomba kura kwa kuwa wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hamad alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalumu kufuatia kitendo cha Lowassa kujitosa kufanya kampeni ndani ya Kanisa la Kilutheri mjini Tabora.
Alisema kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na wananchi kwa kuwa kinakiuka maadili yaliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kushauri ngazi zinazohusika kuchukua hatua kali zaidi kwa mujibu wa sheria ili kukomesha.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa UDP (Zanzibar), Juma Khamis Faki, alimtaka mgombea huyo awaombe radhi Watanzania kwa kitendo hicho.
"Kitendo hicho kimekiuka misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) ya umoja, amani na upendo miongoni mwa Watanzania maana hatuchaguani kwa misingi ya dini zetu wala ukabila," alisema.
Wiki iliyopita akiwa katika ziara ya kampeni mkoani Tabora, Lowassa aliwahutubia waamuni wa kanisa hilo na kuwaomba wamchague kwa kuwa ni muumini mwenzao wa dhehebu hilo hatua iliyoibua hisia miongoni mwa wanajamii, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa karipio kali.
Wakati huo huo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umemtaka Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, kuacha kupotosha umma na kubeza mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.
Umemtaka awe muungwana na msema kweli kuhusu mafanikio yaliyofikiwa ingawa yeye binafsi na chama chake wamekuwa wakichukia hilo.
Pia imemtaka kutoudanganya umma kwa madai kwamba atamudu kuwapa ajira vijana Wanzibari wote katika kipindi kifupi endapo atachaguliwa kuwa Rais.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana na kufafanua kuwa Seif ni kiongozi kigeugeu ambaye hupenda kuudanganya umma na kusema serikali ya umoja huo imeshindwa kufikia malengo yake katika tangu iundwe miaka mitano iliyopita.
“Nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi SUK chini ya Dk. Shein inaongozwa kwa pamoja kisera na mawaziri toka CCM na CUF Maalim Seif akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Uamuzi, ushauri na utekelezaji sera pamoja na mikakati hupitishwa na kutekelezwa katika Baraza la Mapinduzi ambalo Seif pia hushiriki na kushauri,” alisema Shaka.
Aidha UVCCM imemuonya aliyewahi kuwa waziri katika serikali hiyo, Mansour Yussuf Himid, kuacha kutumia msamiati wa 'Mapinduzi daima' katika jukwaa la CUF kwa sababu hayana asili na chama hicho.
"Tunamtaka Mansour aache kutumia neno mapinduzi daima katika mikutano ya CUF, Mapinduzi ya Zanzibar hayana mnasaba wala uhusiano na CUF au ZNP iliongozwa na Ali Mohsin Albarwan.
"Baba yake Mansour Brigedia Yussuf Himid kama ungetokea muujiza wa kufufuka leo angeshangaa kumuona kijana wake akishiriki katika njama za usaliti wa kutaka kufuta mapinduzi aliyoyapigania kwa nguvu zake na kujitolea kuleta ukombozi," alisema.
Kutoka Dodoma, inaripotiwa kuwa Polisi inawashikilia watu wanne ambao ni wafuasi wa CHADEMA kwa tuhuma za kujeruhi na kufanya fujo katika msafara wa mgombea ubunge wa jimbo la Dodoma, Antony Mavunde (CCM).
Kamanda wa Polisi mkoani humo, David Misime, jana, aliwataja watuhumiwa hao kuwa Juma Bika ambaye ni katibu mwenezi wa chama hicho wilaya ya Dodoma Mjini, Fulgence Mapunda, George Mwingira na Deogratias Peter wakazi wa Dar es Salaam.
Misime alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 12.00 jioni, wakati msafara wa CHADEMA ukitoka Uwanja Wabarafu katika kampeni za kumnadi Lowassa na kukutana na msafara wa CCM uliokuwa ukitokea Msalato kwenye mkutano wa kampeni na kuanza kufanya fujo.
Alisema wanachama hao mbali na kufanya vitendo hivyo, pia walifanya uharibifu kwa kuvunja vioo vya magari manne mali ya CCM.
Kamanda huyo alisema wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine ili wote waweze kufikishwa mahakamani.
Misime alisema wanaendelea kuchunguza ili kupata ukweli wa tukio hilo kama kuna wafuasi wengine walitoka Dar es Salaam na walifika Dodoma kufanya nini na kama walibebwa kwa ajili ya kwenda kufanya fujo.
Wakati huohuo, CCM imelaani vikali matukio hayo ya uvunjifu wa amani yanayofanywa na wafuasi wa vyama vinavyounda UKAWA.
Katibu Msaidizi wa Masuala ya Siasa Mkoa wa Dodoma, Othman Dunnga, alisema tukio linaashiria shari inayoanza kujengwa na CHADEMA dhidi ya CCM.
Akizindua kampeni za TLP kwenye Viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam, jana, mgombea urais wa chama hicho, Maximillian Lyimo, alisema UKAWA imejaa unafiki ambao hautaisaidia kuingia madarakani kwa kuwa imeonyesha haina dhamira nzuri na vyama vingine vya upinzani.
Alisema, umoja huo umelenga kuvisambaratisha vyama vingine na kutoa mfano wa jinsi ulivyodhamiria kukimaliza chama hicho ambacho kilikuwa na jimbo moja la uchaguzi, lakini UKAWA unalitaka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment