Mgombea Urais kupitia CCM Dr.John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa mji wa Lamadi kwenye mkutano wa kampeni za CCM |
Mgombea Ubunge jimbo la Busega Dk. Raphael chegeni akihutubia wakazi wa mji wa maji kwenye mkutano wa kampeni za CCM zilizoongozwa na mgombea urais wa CCM Dk. John Pombe Magufuli |
NA SELINA WILSON, BARIADI
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli, amesema akichaguliwa kuwa Rais atakifufua na kukiboresha kilimo cha pamba pamoja na kuweka bei nzuri itakayomnufaisha mkulima.
Amesema serikali itashirikiana na wawekezaji kujenga viwanda vya nguo na nyuzi ili wasiishie kusindika pamba tu na badala yake zitengenezwe nguo na nyuzi za pamba.
Dk. Magufuli alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika wilaya za Bariadi,Busega,Itilima na Meatu alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu.
Alisema kukiwa na viwanda kutakuwa na soko la uhakika la pamba na kwa bei nzuri hivyo aliwataka wananchi wa maeneo hayo wamchague kwa kuwa ameomba urais kwa lengo moja la kuwatumikia wananchi.
Dk.Magufuli alisema ataboresha sekta za kilimo na mifugo ili wananchi hao waishi vizuri na kufanya kazi za uzalishaji.
"Tunahitaji kujenga viwanda vya ngozi, nyama na maziwa. Najua tukiwa na viwanda tutapandisha thamani ya mazao ya mifugo," alisema Dk. Magufuli.
Alisema ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaondokana na migogoro ya ardhi serikali yake itapima maeneo na kugawa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
"Watu na mifugo wanaongezeka lakini ardhi ni ile ile. Wakati tunapata uhuru tulikuwa na ng'ombe milioni tisa lakini sasa kuna ng'ombe milioni 24," alisema.
Alisema kwa kuwa wakulima na wafugaji wote wanahitajika ni vizuri kugawa maeneo ili kila upande ufanye kazi zake kwa ufanisi na kukuza uchumi.
Akizungumzia miundombinu Dk.Magufuli alisema ataunganisha wilaya za mkoa wa Simiyu kwa barabara za lami ili wananchi waweze kufikisha bidhaa zao kwenye masoko.
Dk. Magufuli alisema pia serikali yake itaendeleza programu za kupeleka umeme katika maeneo mbalimba ya wilaya za mkoa huo ikiwemo vijijini ili kuharakisha maendeleo.
Pia alisema serikali itaondoa ushuru na kodi za manyanyaso kwa wafanyabishara ndogo ndogo ili kuwaondolea kero wananchi.
"Ng'ombe wako unapeleka mnadani kumuuza unatakiwa kulipa ushuru wa ajabu ajabu. Unapeleka miwa yako sokoni hakuna aliyekusaidia lakini unatozwa ushuru,"alisena
Akizungumza Mjini Bariadi Mgombea ubunge wa Bariadi Magharibi,Andrew Chenge kwa tiketi ya CCM, alimhakikishia Dk. Magufuli kwamba atapata kura za kutosha za ushindi katika jimbo lake.
Chenge alisema kero kubwa ya wananchi wake ni maji, hivyo alimuomba Dk.Magufuli akiingia Ikulu atekeleze ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kuleta maji kutoka ziwa Victoria.
Kwa upande wake Mgombea Ubunge wa Kisesa Wilayani Meatu, Luhaga Mpina, alimkabidhi nyaraka alizoanisha matatizo ya jimbo lake na kumuomba Dk. Magufuli akiingia Ikulu awasaidie kuzitatua.
Mpina alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni maji,malisho ya mifugo hali inayosababisha ng'ombe kukamatwa na kuwekwa rumande na wakati mwingine wanapigwa risasi na askari wa wanyama pori.
Alimuomba Dk. Magufuli akiingia Ikulu awasaidie kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mwandoya ili kiwe hospitali teule ya wilaya kutokana na mahitaji makubwa ya huduma za afya.
Pamoja changamoto hizo Mpina alimsifu Dk. Magufuli kuwa mchapa kazi ambaye amefanya kazi kubwa wizara ya ujenzi ikiwemo kujenga barabara za lami na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo za Mkoa wa Simiyu.
Akijibu kero hizo, Dk.Magufuli aliahidi kuzifanyia kazi na kuwaomba wananchi wamchague Mpina ni mchapa kazi ambaye atashirikiana naye kumaliza kero za jimbo hill.
No comments:
Post a Comment