Sunday, 13 September 2015
DK. SHEIN KUZINDUA KAMPENI LEO, KIKWETE KUWAAGA WAZANZIBARI
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), leo, kinazindua mikutano ya kampeni za urais kwa kumnadi mgombea wake wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika Viwanja vya Demokrasia (Kibanda Maiti) pamoja na kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2o000 kwa wanachama wake.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, alisema jana kuwa, mkutano huo utahudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete pamoja na Katibu Mkuu wa Chama, Abdulrahman Kinana.
Vuai alisema CCM Zanzibar inazindua kampeni zake huku ikiwa na uhakika na mkubwa wa ushindi baada ya kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi inayomalizika mwaka huu kwa zaidi ya asilimia 90.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo Chama kinajivunia kuyafanikisha kuwa uimarishaji wa zao la karafuu kwa wakulima, ambapo bei imeongezeka na kuwafanya wakulima wapate asilimia 80 ya faida.
"Wakulima wa zao la karafuu sasa wananufaika na nyongeza ya bei pamoja na asilimia 80 inayotolewa faida moja kwa moja ambayo imeleta mabadiliko makubwa," alisema.
Aliyataja mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa uimarishaji wa elimu ya msingi na sekondari ambapo sasa elimu ya maandalizi imefanywa kuwa ya lazima kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi kuwa na uwezo mkubwa darasani.
Mafanikio hayo yanaifanya Zanzibar kuvuka malengo ya milenia ya kuingiza wanafunzi wengi wenye umri wa kwenda shule kupata fursa na haki ya msingi ya elimu. Katika mkutano huo viongozi, waasisi pamoja na marais wastaafu watahudhuria
Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewaomba Wazanzibari kujitokeza kwa wingi wakati CCM ikizindua kampeni zake.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka, alisema uzinduzi huo ni mwanzo rasmi wa safari ya uhakika kurejea tena Ikulu kushika dola kwa awamu nyingine baada ya Dk. Shein kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015.
Alisema uzinduzi huo utakuwa ni wa aina yake kutokana na kusheheni mambo mbalimbali ikiwemo uwepo wasanii wa hapa nchini, wanasiasa na wanamuziki maarufu watakaoburudisha umati utakaojitokeza.
“Leo CCM tunazindua kampeni zetu kwa ajili ya kusaka nafasi ya kurudi tena, wananchi wana imani na sera za Chama chetu. Naomba sote tuhudhurie ili kufahamu vipaumbele vyetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment