NA DOTTO MADUHU, MWANZA
WANANCHI wametakiwa kutogombana na kutoleana lugha ya
matusi kwa sababu uchaguzi mkuu utapita na nchi itabaki.
Wito huo ulitolewa juzi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
CCM (UVCCM) Wilaya ya Ilemela, Herry James, katika mkutano wa kampeni wa
kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Nyamanoro kwa tiketi ya CCM, uliofanyika
katika uwanja wa Ghana.
Alisema kugombana kwa ajili ya siasa husababisha
wahusika kupata ulemavu, kufungwa na kupoteza maisha huku wanasiasa wakiendelea
kula raha bila kuwakumbuka wahusika.
James alisema wanasiasa wengi ni waigizaji na hawana
uadui wa kudumu zaidi ya siasa, lakini katika maisha ya kawaida ni marafiki na
wanashirikiana katika mambo mbalimbali na kuwaacha wananchi wasiojua
wakikwazana kivyao.
"Ngoja niwaambie ndugu zangu, siasa hazina uadui wa
kudumu, kwani viongozi wengi katika maisha ya kawaida wanashirikiana, mfano,
kuna kiongozi mmoja kwa miaka minane alituhumiwa na kuchafuliwa na chama kimoja
cha siasa nchini, lakini sasa wanakaa meza moja na kula pamoja huku wananchi
mkibaki na alama ya mshangao,” alisema.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupigakura
ifikapo Oktoba 25, mwaka huu, bila kufanya vurugu kwa kuwa matokeo yote
watakuwa nayo mawakala wa vyama.
Alisema ni vyema wafanye hivyo ili kujiepusha kupata
ulemavu, kufungwa na kupoteza maisha kwa ajili ya wanasiasa ambao hawawezi
kuwakumbuka.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Kirumba, Wessa
Juma, aliwaomba wananchi hususan vijana kutokubali kutumika kama chambo kisiasa
kwa kuwa watu wengi wamepoteza maisha na kubaki na ulemavu sambamba na kufungwa
huku familia zao zikibaki masikini na wahusika wanaendelea kuishi salama.
“Kuna matukio tofauti yanayohusika na vurugu za kisiasa
yalitokea hapo nyuma nchini huku vijana wengi wakitumika na baadhi yao
wakipoteza maisha, kuwa walemavu na wengine wapo magerezani wakipata tabu,
ingawa wanasiasa waliokuwa wanawatetea hawawajali,” alisema Juma.
No comments:
Post a Comment