Sunday, 13 September 2015

MPUUZENI SUMAYE- MADENGE




Sheila Simba, Tudarco
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kupuuzia maneno yanayotolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kwani, hayana mashiko.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, juzi, katika uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya Kunduchi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, alisema Sumaye na wenzake hawana sera kwani sera ya CHADEMA ilikuwa ufisadi ambayo kwa sasa haipo tena.
Aidha, alisema CCM imejipanga kushika dola na kuwataka wananchi  kumpa kura za ndio mgombea udiwani wa CCM, Michael Urio kwani Chama kina watu imara na ambao wapo tayari kulitumikia taifa.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya Tegeta Nyuki, mgombea udiwani Urio, alisema yupo tayari kutatua kero zinazowakabili wananchi hao kwani anazijua vizuri.
“Naomba mnipe ridhaa ya kuwa diwani wenu ili tushirikiane kutatua kero za kata yetu, kwani nazijua kwa kuwa mimi naishi na nyie huku, kwa ushirikiano wenu tunaweza kufikia malengo,” alisema.
Aliongeza kuwa kata imekuwa na upinzani kwa miaka mitano, lakini hakuna kilichofanyika kwani, wameshindwa kununua hata gari la kubebea wagonjwa na kuchimba mitaro ya kupitisha maji machafu.
Aidha, mgombea huyo alitaja vipaumbele vyake katika kuongoza kata hiyo kuwa ni mazingira safi, kuongeza ajira kwa vijana kwa asilimia tano, huduma safi za jamii, kushughulikia matatizo ya ardhi na kukomesha rushwa katika kata hiyo.

No comments:

Post a Comment