NA ABDALLAH MWERI, MKURANGA
MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga (CCM), anayemaliza muda
wake, Adam Malima, amewataka Watanzania kutokupiga kura za chuki dhidi ya
Chama.
Malima, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni
za mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika
Kijiji cha Kimanzichana mkoani Pwani.
Alisema Watanzania watajutia uamuzi wao endapo watapiga
kura za hasira katika uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu.
Mbunge huyo alisema Watanzania wapuuze kauli za
ubabaishaji zinazotolewa na upinzani kuwa CCM haijafanya lolote tangu
ilipoingia madaraka.
Malima alisema CCM ndio Chama pekee kinachotekeleza
Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo.
“Nawaombeni sana msije mkapiga kura za hasira dhidi ya
CCM, mtakuja kujuta. Ndugu zangu wa Mkuranga mpigieni kura Magufuli, mbunge
wetu, Abdallah Hamis Ulega na madiwani wote 25 wa CCM,” alisema.
Malima, alitoa mfano wa wakazi wa Mbeya Mjini, ambao
walipiga kura za hasira kwa kumchagua Joseph Mbilinyi wa CHADEMA na sasa
wanajuta.
"Mbeya walimchagua mtu anaitwa Sugu, jina lenyewe
tu tatizo. Haya kule Kilwa walimchagua bwege, hivi kweli mbunge anaitwa bwege,”
alihoji.
Alisema CCM imewaletea maendeleo Watanzania katika
nyanja mbalimbali, hivyo hawana sababu ya kupiga kura za chuki.
Mbunge huyo alisema Dk. John Magufuli na Samia ni
viongozi shupavu ambao, watailetea maendeleo nchi katika serikali ya awamu ya
tano.
Pia, alimtaka Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye kuacha
kusema uongo kuwa serikali imeshindwa kuleta maendeleo na aliwataka Watanzania
kumpuuza.
“Huyu mzee wa ajabu sana, nimefanya naye kazi akiwa
waziri mkuu, kama anadai CCM haijafanya kitu basi hata yeye hakuwa lolote,” alisema.
No comments:
Post a Comment