Sunday 13 September 2015

NDIKILO AWAONYA WATAKAOVURUGA UCHAGUZI PWANI




MKUU wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndikilo, ameonya kuwa serikali itachukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayefanya vurugu katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Ndikilo alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika Wilaya ya Rufiji, Pwani.

Ndikilo alisema wanazo taarifa za kiintelejensia kuwa kuna baadhi ya watu wanajiandaa kufanya vurugu katika uchaguzi huo, hivyo ameonya mtu yeyote asithubutu kufanya vitendo vya uhalifu kwa kuwa atashughulikiwa.

"Hatulali tunafanya kazi asubuhi, mchana na usiku. Kwa kweli mtu yeyote asithubutu kufanya vurugu, tutamshughulikia vizuri sana na tumejipanga, naomba wananchi msiwe na hofu, siku ikifika, amkeni mapema mkapige kura, hakuna mtu wa kuwatisha," alisema Ndikilo.

Ndikilo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, alisema serikali imejiandaa kupambana na watu wanaotumika kwa manufaa ya wengine kufanya vurugu.

No comments:

Post a Comment