Sunday, 13 September 2015

KOKA APANIA KUWAINUA VIJANA NA WANAWAKE KIBAHA MJINI




Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kibaha Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Pwani, Silvestry Koka, amesema endapo atachaguliwa kuliongoza jimbo hilo, ataendelea kuwezesha makundi mbalimbali ya vijana na wanawake kwa kuwatengea shilingi milioni 700 kwa ajili hiyo.
Amesema katika kipindi kilichopita, alitumia shilingi milioni 480 kwa kuyawezesha makundi hayo, hivyo kwa sasa amejipanga kuongeza nguvu ili waweze kuinua biashara zao.
Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Mailmoja, Kibaha,juzi,  Koka aliwaomba wananchi wa jimbo hilo waendelee kumuamini ili washirikiane kuinua maendeleo ya jimbo.
Aidha, Koka alisema atatoa shilingi milioni 700 kwa kuviwezesha vikundi  pekee, hivyo aliwataka wajasiliamali wajenge tabia ya kuunda vikundi na kuacha ubinafsi.
"Mimi na mke wangu tumeshirikiana kikamilifu na nyie wananchi katika miaka mitano iliyopita na mtakuwa mashahidi kwa yale ambayo tuliweza kuwaunga mkono.
"Vikundi mbambali hususan vya vijana na wanawake tulivipatia mitaji,ujuzi na elimu ya ujasiliamali, elimu ya kutengeneza batiki na keki, hivyo tutaendeleza harakati hizo, "alisema Koka.
Alisema kwa upande wa vijana, waendesha bodaboda aliwapatia pikipiki 15, katika vikundi vyao ambavyo vipo kwenye kata 14 na pikipiki moja ilikuwa ni ya ofisi ya vijana hao.
Alisema pikipiki hizo ni kama mbegu ambapo inafanya biashara na kipato kinachopatikana wanaweka akiba ya kikundi ili kununua pikipiki nyingine ambazo zitatokana na mbegu waliyopewa.

No comments:

Post a Comment