Sunday 13 September 2015

RIDHIWANI ATANGAZA NEEMA ZAIDI CHALINZE




Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani, kupitia CCM, Ridhiwani Kikwete, amesema endapo wananchi wa jimbo hilo watamchagua kwa kipindi kingine cha miaka mitano, atahakikisha tatizo la maji linakwisha na kuwa historia.
Aidha, amesema katika jimbo hilo wananchi zaidi ya 30,000 wamejiandikisha kupigakura, kati yao 27,000 ni wanachama wa CCM, hivyo ana uhakika wa CCM kushinda kwa asilimia 93, kwa upande wa  mgombea urais John Magufuli,mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan, mbunge na madiwani.
Akizungumza juzi na baadhi ya wananchi wa Chalinze, Ridhiwani alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, alijitahidi kusimamia mradi wa pili wa maji –WAMI Chalinze na mpango huo unaendelea ili kuhakikisha tatizo hilo linakwisha.
Alieleza kuwa alifanikiwa kusimamia kwa kuhakikisha maji yanafika katika makao makuu ya vijiji vyote, ambapo zaidi ya  asilimia 82 ya mahitaji ya maji katika maeneo hayo imefikiwa.
Ridhiwani alisema serikali ya awamu ya nne inayoondoka madarakani iliingia mkataba na serikali ya India wa awamu ya tatu ya mradi wa maji WAMI –Chalinze, wenye thamani ya sh. bil. 420 ili kuhakikisha maji yanafika katika vitongoji vyote vinavyotengeneza vijiji jimboni hapo.
“Kwangu mimi ni faraja kubwa kuwaeleza kuwa nimejitahidi kusimamia awamu iliyopita na sasa kama nitapata ridhaa ya kuendelea kuongoza jimbo la Chalinze, nitahakikisha nasimamia mradi wa awamu ya tatu na fedha lengwa zinatolewa kwa wakati ili mradi ukamilike haraka,”alisema Ridhiwani.
Alisema mradi huo wa maji utakapokamilika, utawezesha maji kufika kwenye maeneo yote na matanki makubwa yanajengwa ili kuhakikisha maeneo ambayo maji yalikuwa yakisuasua, yaweze kufika kwa uhakika.
Alisema anaamini serikali ya awamu ya tano kwa uongozi wa Dk. Magufuli na Samia, iwapo watapata ridhaa ya Watanzania, watashirikiana kusimamia fedha za mradi wa awamu ya tatu WAMI-Chalinze na kuhakikisha zinafika na kufanya kazi husika.
Akizungumzia suala la elimu, Ridhiwani alisema katika kipindi chake, alipeleka vitanda kwenye shule zote za sekondari katika jimbo zima la Chalinze, ili kuondoa tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu na kulala shuleni na kupunguza mimba za utotoni.
Alisema wakati anaingia madarakani, kulikuwa na baadhi ya miundombinu mibovu na kusababisha wanafunzi wengine kulala nje ya shule na kuwepo kwa mimba za utotoni kwa kiasi kikubwa, ambapo alihakikisha anaboresha miundombinu na kupeleka vitanda hivyo.
Ridhiwani alisema bado ipo changamoto ya kuimarisha miundombinu ya madarasa,mabweni na nyumba za walimu na bado wanaendelea kukabiliana na changamoto hiyo. Alisema kwa sasa wamejenga majengo zaidi ya 30 ya walimu katika shule ya sekondari ya Lugoba

No comments:

Post a Comment