NA
PETER KATULANDA, ITILIMA
MGOMBEA
ubunge wa CCM katika jimbo la Itilima, mkoani Simiyu, Njalu Silanga, amemuahidi
maendeleo makubwa mgombea urais wa Chama,Dk. John Magufuli iwapo watachaguliwa
na wananchi.
Ameahidi
kuwa iwapo Dk. Magufuli anataka ‘kazi tu’, yeye atakuwa ni mbunge wa ‘vitendo
tu’ ili maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo mpya yapae.
Majibu
ya ahadi hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano wa hadhara
wa kampeni za CCM katika Kijiji cha Nanga, wilayani humo, yalipotolewa na Dk.
Magufuli, yalikonga nyoyo za mamia ya wananchi hao waliopaza sauti kuomba
wambebe huku wakiwaahidi kura za kishindo.
“Mheshimiwa
mgombea urais Dk Magufuli najua wewe ni kipenzi cha wananchi, wengine
wanashiriki tu uchaguzi, mimi tayari nakuita Rais mteule,” alisema Silanga na
kuufanya umati wa wana Itilima uzizime kwa shangwe na kukubaliana naye kuwa
huyo ndiye rais wanayemhitaji awamu ijayo.
“Tuna
matatizo makubwa ya barabara, maji safi na salama ya kunywa, mabwawa na malisho
ya mifugo yetu, tunajua wewe ni mtu wa sheria, uje ulishughulikie hilo, watu
wanateseka, hawana marisho, watumishi hawana nyumba,” aliomba mgombea huyo.
Silanga,
ambaye aliahidi pia kuboresha huduma za jamii na kuwapiga jeki vijana,
alifafanua kuwa, wananchi wa wilaya hiyo wamekosa malisho ya mifugo kwa sabau
ya mgogoro ulioshindikana kutatuliwa baina yao na pori la Hifadhi ya Akiba ya
Maswa, hivyo wanaamini atakapokuwa rais kero hiyo itatatuliwa mara moja.
Mgombea
huyo alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuanzisha wilaya hiyo ili kusogeza
karibu huduma za wananchi na kuondoa michango mbalimbali iliyokuwa kero kwa
wananchi na sasa CCM imepania kutoa elimu ya msingi hadi kidato cha nne bure.
Akijitambulisha
na kuomba kura kwa Wana-Itilima, Dk. Magufuli alimfagilia Silanga kwa kumuahidi
kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, ambayo
itatatua kero hizo.
“Barabara
zenu na daraja nimeziona, nawaahidi ndugu zangu nikiwa rais, nitayatekeleza na
kuijenga wilaya hii mpya ikiwa pamoja na nyumba za watumishi, suala la mpaka
nitalishughulikia mara moja ili mpate malisho,” alisema.
Dk.
Magufuli alihoji atashindwaje suala la mipaka ya ardhi akiwa rais wakati rais
ndiye mwenye mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi na kuwafanya tena
wananchi hao wamshangilie na kumuomba kwa lugha ya kisukuma wambebe (kama
heshima) na ishara ya kutukuka.
“Mnataka
kunibeba ?” Aliwauliza.
“Ndiyo,” walijibu na Dk. Magufuli akawashukuru
na kuwaomba wambebe kwa kumpigia kura za ndiyo nyingi, ikiwa ni pamoja na
wagombea wote wa udiwani na ubunge wa CCM na kwamba wasipofanya hivyo, hata
kama wakimbeba mgongoni haina maana na matumaini yao yatapotea bure.
No comments:
Post a Comment