Sunday, 13 September 2015

156 WAIHAMA UKAWA NA KUJIUNGA NA CCM





Na Mwandishi wetu, Tabora

WANACHAMA 156 kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamevihama vyama vyao na kutimkia CCM, wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani zilizofanya jana katika kata ya Cheyo mjini Tabora.

Wanachama hao wamedai kuwa UKAWA hawana jipya katika siasa kwani
wameshindwa kusimamia misingi ya utawala bora na mabadiliko kwa
kuwaingiza viongozi wanaotuhumiwa katika ufisadi na kukosa uzalendo
kwa Taifa lao.

Walisema malengo ya UKAWA ilikuwa kuleta mabadiliko ya kiutendaji,
kimaadili na utawala bora  pamoja na kulitafutia ufumbuzi suala la
ufisadi linalotafuna taifa na wananchi wake, lakini malengo hayo sasa
hawawezi kuyafikia kutokana na kitendo cha kuwakaribisha wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi.

Mmoja wa wanachama hao waliohamia CCM, ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA, Kata ya Cheyo, alisema wameamua kurudi CCM kwa kuwa ndicho chama pekee ambacho kwa sasa kinaweza kuleta mabadiliko chini ya mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli.

Awali, mgombea ubunge wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka, aliwashangaa baadhi ya mawaziri wakuu waliokihama chama hicho baaada ya kuenguliwa kwenye kinyang’anyilo cha kupeperusha bendera ya CCM na kuhamia UKAWA, jinsi wanavyokishambulia licha ya kupewa madaraka makubwa, lakini wakashindwa kuyatumia kwa kuleta mabadiliko.

Alisema kama mtu amekuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka kumi na
hakuleta mabadiliko yoyote ya kijamii, kielimu, kiuchumi, hata
miundombinu, licha ya kuishia kashfa za kujilimbikizia mali, iweje leo hii
anataka kuwadanganya Watanzania kuwa anaweza kuleta mabadiliko? Alisisitiza kuwa huo ni uongo mtupu.

“Hakuna mkoa ambao ulipata bahati ya kutoa mawaziri wakuu watatu kama Arusha, hiyo ni bahati kubwa, viongozi hao walipaswa kutoa shukrani za pekee kwa Chama na serikali, siyo kugombania madaraka ya juu tena kwa kutumia nguvu nyingi. Yatupasa kujiuliza wanatafuta nini?” Alihoji Mwakasaka.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Cheyo, Yusuph Kitumbo, aliahidi kumaliza matatizo yote yanayowakabili wananchi wa kata hiyo kwa kukamilisha jengo la zahanati na kufanya mpango wa
kujenga kituo cha afya ili kumaliza kero ya huduma za afya.

Alisema anafahamu vyema kiu ya watu wa Cheyo na kubainisha kuwa
atalivalia njuga suala la elimu na kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye  madawati.

Mgombea huyo pia aliahidi kukarabati madarasa na majengo ambayo hayapo kwenye kiwango cha kuridhisha huku akiomba
ushirikano baina ya wananchi na wadau wa wote wa elimu katika kata
hiyo.

Aidha, aliahidi kujenga kituo cha polisi katika kata hiyo ili kuimarisha suala zima la ulinzi na usalama kwa raia na mali zao, jambo ambalo alisema atalitekeleza ndani ya miezi mitatu iwapo wananchi wa kata hiyo watampa ridhaa ya kuwa diwani wao.

No comments:

Post a Comment