Sunday 13 September 2015

TUTAREKEBISHA USHURU WA KITANDA-SAMIA


 Baadhi ya viongozi wa CCM wakiwa kwenye mkutano wa kampeni wa Mama Samia jibo la Mkuranga

 Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM Mama Samia akiteta jambo na Mgombea Ubunge jimbo la Kibiti, Ally Ungando katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo atika jimbo hilo

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ya awamu ya tano itarekebisha ushuru wa kitanda kwa wakazi wa Kibiti na Rufiji, Mkoani Pwani.

Samia alisema changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa Kibiti na Rufiji ni ushuru wa kitanda, ambao umekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara hususani vijana.

Mgombea mwenza alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika juzi, kwa nyakati tofauti katika wilaya mpya ya Kibiti na Rufiji.

"Nilikuwa nanong'ona na viongozi wenu, nimeambiwa changamoto kubwa inayowakabili hapa ni ushuru wa kitanda, haiwezekani mtu anatengeneza kitanda kwa sh. 80,000, halafu ushuru analipa sh. 120,000 tutaangalia suala hili," alisema Samia.

Alisema vijana wengi wa Kibiti na Rufiji wamejiajiri kwa kutengeneza vitanda, hivyo serikali ya awamu ya tano itaangalia ushuru unaotozwa na Maliasili ili kutoa fursa kwao kupata kipato ambacho kitaleta ustawi katika maisha yao.

Samia, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Muungano), alidokeza kuwa Maliasili ina lengo zuri la kuweka kiwango kikubwa cha ushuru ili kulinda uvunaji holela wa miti.

Alisema serikali ya awamu ya tano inatarajia kujenga viwanda vidogo vya kubangua korosho ambavyo vitakuwa na manufaa kwa vijana wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji kupata ajira.

Alisema mbali na vijana kupata ajira, pia wakazi wa mkoa wa Pwani na Kilwa watapata fursa ya kujiajiri kwa kuwa watauza kwa lengo la kupata kipato na kuinua uchumi wa maisha yao binafsi.

"Serikali ya awamu ya tano itajenga viwanda vidogo vidogo vya kubangua korosho. Vijana wengi watapata ajira na watainua hali zao za maisha kwa kuwa sasa watauza korosho zao katika hali ya ubora," alisema Samia.

Samia, amewataka wakazi wa Kibiti na Rufiji kumchagua Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano ili kupokea kijiti kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.

Alisema kuwa Dk. Magufuli ni mchapakazi na hataki mchezo katika kazi na alitoa mfano akiwa Waziri wa Ujenzi, amewatimua makandarasi walioshindwa kwenda na kasi ya ujenzi wa barabara na madaraja.

Wakati huo huo, Samia aliendelea kupokea wanachama wapya kutoka vyama vya CUF na CHADEMA waliorejea CCM, baada ya kuchoshwa na ubabaishaji wa viongozi wao.

Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia akihutubia mkuano wa kampeni uliofayika Kibiti mkoa wa Pwani

Samia awaonya watumishi wanaoiba dawa hospitali

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema watumishi wanaoshiriki kuiba dawa za hospitali, wajiandae kufanya kazi zingine baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Samia amesema serikali ya Dk. John Magufuli, itaweka mfumo mpya wa kutumia kompyuta kutoa dawa Bohari Kuu ya Madawa (MSD), utakaokuwa mwarobaini kwa watumishi wasiokuwa na maadili.

Mgombea mwenza amesema mfumo huo utadhibiti mianya ya utoaji dawa kwa njia za panya unaofanywa na watumishi wa hospitali mbalimbali nchini.

"Tutakuwa wakali sana katika serikali ya awamu ya tano, wale wote ambao wamekuwa na tabia ya kuiba dawa kuzipeleka katika maduka yao watakiona baada ya Dk. Magufuli kuingia madarakani," alionya Samia.

Samia alisema baadhi ya watumishi wa hospitali wamekosa uzalendo na wamekuwa mstari wa mbele kunyanyasa wagonjwa kwa ajili ya manufaa binafsi ya kupata fedha kinyume na utaratibu.

Akionyesha kukerwa na tabia hiyo, Samia ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alisema inasikitisha kuona mgonjwa anakwenda hospitali kupata matibabu, lakini anaandikiwa dawa na kuambiwa akanunue duka la jirani ambalo linamilikiwa na mtumishi wa serikali.

Alisema serikali ya Dk. Magufuli, itakuwa makini na watumishi waliokosa maadili katika utendaji wa kazi na haitasita kuwatimua watumishi wazembe ambao wamekuwa vinara wa kuipaka matope CCM kwa Watanzania.

Samia alisema mbinu wanazofanya watumishi hao kuiba dawa na kuzipeleka katika maduka yao binafsi zitafikia mwisho baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Wakati huo huo, Samia, amesifu kazi nzuri ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Mbunge wa Rufiji anayemaliza muda wake, Dk. Seif Rashid baada ya kuiongoza vyema wizara hiyo nyeti.

"Jamani lazima niseme ukweli Dk. Rashid amefanya kazi nzuri sana katika Wizara ya Afya, hivi kwa sasa mnaona kuna migomo? Hii yote imetokana na kazi nzuri ya waziri wenu,"alisema Samia.

Kwa upande wake, Dk. Rashid, aliwataka wakazi wa Rufiji kumpa kura za kishindo Dk. Magufuli, ambazo zitatoa fursa kwa Samia kushika wadhifa wa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke nchini.

No comments:

Post a Comment