Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa chama cha United Democrat Party Taifa
(UDP), John Cheyo, amesema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hana uwezo
wa kuleta mabadiliko nchini.
Amesema mwanasiasa huyo ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya
kampuni ya kufua umeme ya Richmond, alikuwa na wadhifa wa juu nchini, lakini hakuweza kufanya mabadiliko yoyote hadi
alipojiuzulu.
Cheyo, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Itilima
mkoani Simiyu, ameonyesha kumuungana mkono mgombea urais wa CCM, Dk. John
Magufuli.
Akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake
zilizofanyika Uwanja wa Mpira wa Kikapu mjini hapa, Cheyo alisema sera yake na
chama chake ni kuhakikikisha elimu inatolewa bure kuanzia chekechea hadi kidato
cha nne.
Mbali na sera hiyo mbunge huyo alisema kuwa ikiwa wananchi
watawapatia ridhaa wagombea ubunge na udiwani wa chama chake, kila kijiji
kitapatiwa fedha kwa ajili ya maendeleo ya vijana na kina mama.
Sera hizo zilizotangazwa na Cheyo, zimekuwa zikinadiwa
katika maeneo mbalimbali nchini na Dk. Magufuli.
Aidha, Cheyo ameonekana kushangazwa na kauli za Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Lowassa kuwa wataboresha kilimo cha pamba,
hali aliyoeleza kuwa ni kudanganya wakulima wa zao hilo.
“Viongozi hawa ni wa ajabu sana…Sumaye amekuwa Waziri Mkuu
kwa miaka 10 alikuwa wapi kuboresha…mbona alishindwa? Lowassa amekuwa waziri
mkuu pia mbona alishindwa?...wakati wakiwa viongozi walisema kuwa hawawezi
kuongeza bei ya pamba kutokana na zao hilo kuwa ushirika…sasa leo
wataboreshaje?...hao hawastahili uongozi
hao,” alisema.
No comments:
Post a Comment