Thursday 3 September 2015

LOWASSA SASA ATUPIWA MAKOMBORA KILA KONA


 
Asumpta Mshana
Angella Kairuki


NA EPSON LUHWAGO, MPWAPWA
WAZIRI Mkuu wa zamani na mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, amezidi kushambuliwa na safari hii ameelezwa kuwa ni mtu asiyejua sheria.
Wakati mwanasiasa huyo akichambuliwa hivyo, mbunge wa zamani wa Nkenge, Asumpta Mshama, amesema anajiandaa kumfikisha Lowassa mahakamani kumtaka aeleze alipo aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Daudi Ballali.
Naye Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alisema wapinzani wanafanya mchezo wa kuigiza kwani walichokifanya kwa kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea ni sawa na kumsilimisha mtu asubuhi na jioni kumteua kuwa sheikh wakati hajui hata aya moja ya Kurani.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika wilayani Mpwapwa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Angellah Kairuki, alisema mwanasiasa huyo ameonyesha kuwa ‘mbumbumbu’ wa sheria.
Alisema hayo kutokana na kauli aliyoitoa Lowassa hivi karibuni kwamba akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha anamtoa gerezani mwanamuziki maarufu, Nguza Viking, anayetumikia kifungo cha maisha kutokana na makosa ya kulawiti.
“Huyu ni mtu anayetaka kuwa Rais wa Tanzania, lakini hajui sheria. Anasema atamtoa Babu Seya (Nguza) iwapo ataingia Ikulu, ina maana kuwa ataingia kuvunja sheria na kuingilia mihimili mingine ya dola. Hafai kabisa kuwa Rais,” alisema.
Alisema Tanzania inaongozwa na utawala wa sheria, lakini inashangaza mtu anayetaka kuwa kiongozi wa nchi kutoheshimu utawala bora.
Kwa mujibu wa Angellah, Watanzania wanapaswa kuwa macho na wanasiasa ambao wana uchu wa madaraka na wanaanza kutoa vitisho kuwa wakiingia Ikulu, watavunja sheria.
“Kila wizara aliyoongoza alisababisha matatizo na migogoro mingi. Hatuna muda wa kuyazungumza mabaya yake lakini niseme inatosha kwani hata Wizara ya Ardhi ambako mimi ni Naibu Waziri alifanya madudu kibao,” alisema.
Angellah alisema Watanzania wanapaswa kuichagua CCM kwa kuwa ina mipango na malengo mazuri kwa ajili ya kuwaletea Watanzania maendeleo, tofauti na wapinzani ambao wanasema sera yao kubwa ni kuitoa CCM madarakani.
“Hivi leo mahitaji ya Watanzania ni kuing’oa CCM madarakani? Wananchi wanahitaji maji, umeme, afya na barabara ambavyo ni ahadi na mipango ya CCM. Chagueni CCM ndiyo mpango mzima,” alisisitiza.

ASUMPTA ACHARUKA
Wakati Angellah akimwonyesha Lowassa hajui sheria, Asumpta Mshama alisema anajiandaa kumfikisha mahakamani kwa kauli zake za utatanishi kuwa atamleta Ballali Tanzania.
“Sisi tunajua kuwa Ballali alishakufa, lakini inashangaza kuona kuwa mtu anasema atamleta. Hii ina maana kwamba Ballali yuko hai, hivyo tunataka atueleze aliko.
“Huwezi kusema kitu kama hiki kama huna uhakika. Inaonekana mwenzetu anajua aliko, sasa amlete na asipomleta nitakwenda mahakamani kumtaka afanye hivyo. Natafuta mwanasheria ili kufungua kesi,” alisema katika mikutano iliyofanyika juzi na jana Mpwapwa na Kibakwe.
Sambamba na hilo, Asumpta alisema Watanzania wanapaswa kuichagua CCM kwa kuwa haina ukanda wala udugu tofauti na CHADEMA ambacho ni chama cha kifamilia.
Kwa mujibu wa Asumpta, CHADEMA ilianzishwa kama chama cha kufa na kuzikana kwenye ukoo wa Mzee Edwin Mtei, lakini baadaye alikigeuza kuwa chama cha siasa.
“Alipoamua kustaafu alimwachia Freeman Mbowe ambaye ni mkwe wake. Mzee Ndesamburo ana mtoto, Lucy Owenya, ambaye ni mbunge na Grace Kiwelu pia ni mke wa mtoto wa Ndesamburo.
“Kama haitoshi, viongozi wengi wa CHADEMA wanatoka kaskazini. Hata waliohamia juzi (Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye) ni wa kutoka kaskazini. (Lawrence) Masha naye ambaye amejiunga na chama hicho mke wake ni wa kutoka Kilimanjaro. Watanzania hatutaki masuala ya ukanda kwani sote ni wamoja,” alisema.


No comments:

Post a Comment