Thursday 3 September 2015

DK. MAGUFULI: NITAZIBA MIANYA YA KUKWEPA KODI





 

NA SELINA WILSON, MTWARA
MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akichaguliwa kuwa Rais, serikali itaongeza makusanyo ya kutoka sh. bilioni 900 hadi mara mbili zaidi.
Amesema serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilipoingia madarakani ilikuwa inakusanya sh. bilioni 300 kwa mwaka na sasa imefikia sh. bilioni 900, hivyo ataongeza mara mbili zaidi.
Dk Magufuli alisema hayo jana mjini Mtwara mbele ya umati wa wananchi waliofurika ndani na nje ya Uwanja wa Mashujaa.
Alisema anajua makusanyo yapo, lakini baadhi ya watendaji wanahujumu, hivyo atahakikisha anasimamia vizuri na kudhibiti uvujaji wa mapato kwa kuwa na uzoefu wa miaka 20 serikalini na anajua kila kona.
Aliwataka wakazi wa Mtwara kumchagua awe Rais wa awamu ya tano kwa kuwa ana malengo ya kuleta maendeleo kwa kutumia wawekezaji wa ndani na nje kwa kujenga viwanda na kumaliza tatizo la ajira kwa asilimia 40.
Pia, Dk. Magufuli alisema wazawa watashirikishwa kikamilifu katika kuendeleza rasilimali za gesi, mafuta na madini ili nao wafanye biashara bila kubaguliwa.
Alisema serikali yake itajenga mtandao wa reli ya kisasa kutoka Mtwara/Songea mpaka Mbamba Bay na itaunganishwa na Liganga na Mchuchuma ili watu wafanye biashara na atapanua Bandari ya Mtwara ili mizigo ya Malawi na Zambia itumie bandari hiyo na kusafirishwa kwa reli hiyo bila kupitia Dar es Salaam.
MABADILIKO YASIYO NA MPANGO
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wasikubali kurubuniwa na matapeli wa kisiasa ambao wamekuwa wakiongopa kwamba wanaweza kuleta maendeleo kwa siku moja.
Aliwafananisha wanasiasa hao sawa na wanaume wanaowarubuni wasichana kwamba wakikubali kuchukuliwa nao watapata kila kitu wakati hata kitanda hana.
Dk. Mafuguli alisema wamekuwa wakisema kuwa CCM imechoka ing`olewe ili wao walete mabadiliko jambo ambalo si sahihi kwa kuwa mabadiliko bora yanaweza kupatikana ndani ya CCM.
Aliwataka wananchi wasikubali kutupa kitanda chenye kunguni na badala yake wasafishe kwa kuwaua kunguni na kuendelea kulalia kitanda.
“Ndugu zangu mimi ndio kiboko yao. Nimegombea ili nisafishe kunguni. Mimi ndio maji ya moto kwa ajili ya kuwaua kunguni wote kwenye kitanda CCM, Msikubali mabadiliko yasiyo na mpango,” alisema.
Alisema Tanzania inahitaji mabadiliko na mabadiliko hayo yataletwa na yeye na ndio maana alipoteuliwa tu, mafisadi wanaochafua chama wameanza kukimbia wenyewe.
Dk. Magufuli ambaye alipanda jukwaani saa 10:12 jioni, alisema hatasahau mapokezi hayo na anaamini kwamba umati huo unaonyesha dalili kwamba wanataka mabadiliko na yeye amegombea urais kwa ajili ya kuleta mabadiliko bora.
Kwa upande wa majeshi, alisema anakerwa na uvamizi kwenye vituo na kuhoji majambazi na kuhoji mbona hawavamii kambi za JWTZ wala Ukonga FFU.
Dk. Magufuli alisema anajua wanaogopa cha moto, hivyo alisisitiza kwamba kwenye serikali yake anataka kujenga nidhamu ya jeshi la polisi.
Pia, alisema serikali yake itaangalia walemavu wa aina zote  ili kuhakikisha wanapata haki zao na kuendesha maisha yao.

LUKUVU ASEMA ALIPITA MCHUJO HALALI
Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu, William Lukuvi aliwapongeza wananchi wa Mtwara kwa kufurika kwa wingi katika Uwanja wa Mashujaa kumpokea na kumsikiliza mgombea wa CCM Dk. Magufuli.
Akimtambulisha Dk. Magufuli, Lukuvi alisema ni kada aliyepita kwenye mchujo wa machakato halali wa uchaguzi wa ndani ya CCM na kupitishwa kwa kura nyingi.
Aliwataka wananchi wa Mtwara wahoji, wagombea wengine walipita kwenye mchujo gani na waeleze katika mchakato walikuwa wangapi mpaka akateuliwa mmoja.
Lukuvi alitoa mfano wa kada wa CCM aliyekatwa na kutimkia UKAWA kwamba aligombea nafasi hiyo kwa kushindana na nani na kwenye mchujo walikuwa wangapi.
Alisema Dk. Magufuli ni kiongozi aliyefanya kazi ndani ya serikali na kazi yake imeonekana nchi nzima na ndio maana CCM imemsimamisha baada ya kushinda kwa vigezo mbalimbali ndani ya Chama.
MAGUFULI MWADILIFU – MPANGU  
Kada wa CCM na Katibu Mkuu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Amon Mpanju, amesema Tanzania inahitaji Rais makini, muadilifu na mwenye kuchukia ufisadi.
Mpanju akihutubia mamia ya wananchi wa Mtwara Mjini, alisema vijana wasikubali kupotoshwa wakachagua Rais fisadi ambaye ameghubikwa na kashfa.
Alisema wakitoa fursa kwa mtu wa aina hiyo watatengeneza serikali itakayoongozwa na genge la mafisadi, hivyo chaguo sahihi ni Dk. Magufuli wa CCM.
Katika hatua nyingine, alimpongeza aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kwa kuwa mzalendo wa kweli na kuzungumza hadharani juu ya ufisadi wa mgombea urais wa wa UKAWA, Edward Lowassa.
Alisema kitendo cha Dk. Slaa kueleza kujitenga na siasa kutokana na CHADEMA kumsimamisha mtu anayetuhumiwa kwa ufisadi kuwania urais ni kitendo cha kishujaa na kizalendo.
Katika hatua nyingine, Mpanju alivionya vyombo vya habari vinavyotuhumiwa kununuliwa na wanasiasa ambavyo vimekuwa vikiandika habari za upendeleo kwa baadhi ya wagombea na wakati mwingine kupotosha wananchi.
MURJI ATAMBA KERO SASA BASI
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Mtwara Mjini, Hasnein Murji, alisema kero kubwa za wana Mtwara ni ajira kwa kuwa baadhi ya wenye viwanda hawatoi ajira na badala yake wanakwenda na watu wao.
Murji alisema baadhi ya watu wanaoporwa ardhi yao na wawekezaji bila kulipwa chochote jambo ambalo limekuwa kero kubwa.
Alisema ana amini chini ya utawala wa Dk. Magufuli ambaye hana kashfa ya ufisadi, anajua changamoto zote zitapatiwa majibu na wananchi watanufaika na rasilimali zao.
Akijibu kero hiyo, Dk. Magufuli alisema sheria za ardhi zipo wazi, hakuna mwekezaji au serikali inayoruhusu kuchukua ardhi ya mtu bila kulipwa fidia. Alisema suala hilo amelichukua na atalifanyia kazi.
Pia, Dk. Magufuli aliwapokea wanachama 51 kutoka CHADEMA wakiongozwa na  aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Mtwara, George Makota.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Makota alisema wameamua kuondoka CHADEMA baada ya kuona hakuna maendeleo na maendeleo ya kweli yapo ndani ya CCM.
APAGAWISHA NA YAMOTO BAND, CHEGE
Dk. Magufuli katika kujinadi kwa wana Mtwara aliwapagawisha pale alipopanda jukwaani na kuanza kucheza sambasamba na vijana wanaounda kundi la Bendi ya Yamoto .
Aliamsha kelele za shangwe pale alipopanda jukwaani kwa mara ya pili na kucheza wimbo wa Mkono Mmoja wa nyota wa kundi la Wanaume Family, Juma Said (Chege).
Huku akionyesha kuendana na midundo na mziki uliokuwa ukiimbwa na kusababisha wanananchi waliofurika katika Uwanja wa Mashujaa kumshangilia vilivyo.
Yamoto Bendi ilianza kutumbuiza wakati Dk. Magufuli akiingia uwanjani hapo na ghafla alipanda jukwaani na kuanza kuimba na kucheza wimbo wa Baba Huyoooo.
Wimbo huo ambao ulikuwa ukiimbwa na msanii wa kundi hilo, Maromboso umeingizwa maneno yanayomtaja Dk. Magufuli na kuisifia CCM.
Kutokana na mvuto wa wimbo huo na kitendo cha Dk. Magufuli kucheza, wananchi waliofurika uwanjani hapo wazee kwa vijana walionekana wakicheza na kushangilia.
Akicheza wimbo wa Chege, Dk. Magufuli aligeuza kofia yake na kuanza kucheza huku akiweka mkono mmoja juu ili kwenda pamoja na mashairi ya wimbo huo.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Dk.Magufuli alisema atadhibiti wizi wa kazi za wasanii na uonevu wa kila aina dhidi yao.
Dk. Magufuli alisema atanzisha mfuko kusaidia wasanii ili waweze kunufaika na kazi wanazofanya.

No comments:

Post a Comment