Thursday 3 September 2015

MTERA KUWA NA HALMASHAURI YAKE-SAMIA





NA EPSON LUHWAGO, MTERA
SERIKALI ijayo ya CCM inakusudia kuanzisha halmashauri katika jimbo la Mtera mkoani Dodoma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupeleka madaraka karibu na wananchi.
Sambamba na halmashauri, pia kiwanda cha kutengeneza mvinyo kitajengwa ili kuongeza thamani ya zabibu zinazozalishwa katika jimbo hilo.
Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Mlowa Barabarani.
Samia alitoa ahadi hiyo kutokana na ombi la Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, aliyesema Wilaya ya Chilonwa ni kubwa jambo linalokwamisha maendeleo kwa kuwa kuna halmashauri moja tu ya wilaya.
Pia, alisema wananchi wa Mtera ni wakulima wazuri wa zabibu,  lakini wanaziuza kwa hasara kutokana na kutokuwa na kiwanda cha kutengeneza mvinyo.
Akijibu maombi hayo, mgombea mwenza alisema serikali ijayo inatarajia kufanya hayo yote ili kuwezesha utoaji wa huduma. Alisema suala la kiwanda cha kutengeneza mvinyo liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka huu.
“Hili suala la kiwanda halina mjadala kwa sababu Ilani ya Uchaguzi inalizungumzia. Tutahakikisha kiwanda cha mvinyo kinajengwa ili kuongeza thamani ya zao la zabibu. Kiwanda hiki kitawezesha kuwepo kwa soko la uhakika la zabibu zenu,” alisema.

No comments:

Post a Comment