Thursday, 10 September 2015

UKAWA WAIGIZAJI-JANUARY MAKAMBA



NA SELINA WILSON, BUMBULI

MJUMBE wa Kamati ya Kampeni za CCM na mgombea ubunge wa jimbo la Bumbuli, January Makamba, amesema UKAWA wanafanya mazingaombwe kwa kuwalamisha wananchi wazungushe mikono yao kuashiria mabadiliko.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa makini na mtindo huo wa mazingaombwe kwani zipo kumbukumbu za mataifa yaliyofanya mazingaombwe kwa zaidi ya miaka 20,  maisha ya wananchi wake hayajabadilika.

January aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bumbuli na kuhudhuriwa na umati wa wananchi.

“Ndugu zangu wanapowaambia mkunje ngumi halafu mzungushe mikono, wanawafanyisha mazingaombwe bila nyie kujijua na matokeo ya mazingaombwe hayajawahi kuwa na manufaa kwa wananchi,”alisema.

Alisema wananchi wa Zambia wamewahi kufanya mazingaombe na kubadilisha viongozi mara kwa mara hadi walipomchagua Michael Satta, lakini maisha ya wananchi hayajawahi kubadilika.

January aliwataka wananchi wa Bumbuli kumchagua Dk. Magufuli kwa kuwa ndiye atakayeleta mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo kwa Watanzania.

Akizungumzia kiwanda cha Mponde , January alisema serikali imeshakirudisha kwa wananchi, lakini wanakwamishwa na kitu kinachoitwa mchakato, hivyo walimuomba Dk. Magufuli akiingia madarakani akabidhi kiwanda hicho ili kianze kufanya kazi.

Alimuhakikishia Dk. Magufuli kwamba kura zote za Bumbuli atazipata kwa vile wananchi wana imani naye na ndio maana juzi alipofika mgombea mwenza wa UKAWA, Juma Duni Haji, alipata wananchi 40 tu katika mkutano wa hadhara.

Akijibu ombi hilo, Dk, Magufuli alisema serikali yake ni ya kutekeleza mambo, hivyo atahakikisha anazifanyia kazi kero zote na kuhakikisha wananchi wanaishi mazisha mazuri.

Aliwataka wananchi wa Bumbuli wamchague January kwa kuwa ni kijana aliyetulia na mwenye moyo safi wa kuwatumikia wananchi wake.

No comments:

Post a Comment