Thursday, 29 October 2015

DK JOHN MAGUFULI RAIS MPYA WA TANZANIA


HATIMAYE Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza matokeo rasmi ya kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,mwaka huu.

Akitangaza matokeo hayo kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, leo jioni, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alimtangaza mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Dk. Magufuli ameibuka mshindi baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46, akifuatiliwa na mgombea wa CHADEMA, Edward Lowassa, aliyepata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.93

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Anna Elisha Mghwila ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 98,763, sawa na asilimia 0.65, akifuatiwa na Chifu Lutalosa Yemba wa ADC, aliyepata kura 66,049, sawa na asilimia 0.43 na Hashim Rungwe Spunda wa CHAUMA, aliyepata kura 49,256 sawa na asilimia 0.32.

Wagombea wengine walikuwa Lyimo Macmillan Elifati wa TLP aliyepata kura 8, 198, sawa na asilimia 0.05, Kasambala Janken Malik wa NRA, aliyepata kura 8,028, sawa na asilimia 0.05 na Dovutwa Fahmi Nassoro wa UPDP, aliyepata kura 7,785 sawa na asilimia 0.05.

Kutokana na matokeo hayo na kwa mujibu wa madaraka aliyonayo kikatiba, Jaji Lubuva, alimtangaza rasmi Dk.Magufuli kuwa ndiye Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2015/2020. Dk. Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5, mwaka huu.

Mbali na mgombea wa CCM kushinda kiti cha urais, pia Chama kimeshinda majimbo 204 ya uchaguzi kati ya majimbo 264 na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikilinganishwa na wapinzani.

Kwa mujibu wa NEC, uchaguzi wa wabunge katika majimbo mengine saba haukufanyika, sita kutokana na vifo vya wagombea wa vyama vya CCM na CHADEMA vilivyotokea wakati wa kampeni na pia kujitokeza kwa baadhi ya kasoro chache.




No comments:

Post a Comment