Wednesday 28 October 2015

KANGI LUGOLA AMCHAKAZA MPINZANI WAKE




Na Ahmed Makongo, Bunda
MGOMBEA ubunge katika jimbo la Mwibara, kupitia tiketi ya CCM, Kangi Lugola, maarufu Kangi Bomba Nati ya Kirumi, ametetea nafasi yake baada ya kumshinda mgombea wa CHADEMA, aliyewahi kumshinda tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Msimamizi wa Uchaguzi katika Wilaya ya Bunda, Lucy Msoffe, alimtangaza jana Lugola kuwa mshindi kwa kupata kura 33,845 na kumshinda Chiriko Haruni wa CHADEMA aliyepata kura 6,675.
Msimamizi huyo wa uchaguzi katika jimbo la Mwibara, pia alimtangaza mgombea mwingine kuwa ni Mtamwega Mgaywa wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 521.
 Hata hivyo, mgombea huyo alisikika akisema kuwa alikuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho, licha ya wananchi kumpigia kura bila ya yeye kuwepo wala kufanya kampeni.
 Akizungumza na waandishi wa habari baada ya matokeo hayo kutangazwa, Lugola alisema kuwa aliamini kuwa ataibuka na ushindi mkubwa kwa sababu ya utendaji kazi wake mzuri.
Alisema kuwa atawatumikia wananchi wa jimbo hilo kama kawaida yake, maana anautambua mchango wao wa kumwamini tena kuendelea kuwa kiongozi wao katika uchaguzi wa mwaka huu uliokuwa na ushindani mkubwa.
Aidha, alisema atapigania jimbo la Mwibara kuwa na halmashauri na wilaya yake ili kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.
 “Madiwani wa huku juu wakae mkao wa kujitathmini maana tunataka Mwibara nayo iwe halmashauri na wilaya.
 “Tena mimi nitamsaidia mgombea wetu wa urais ambaye nina amini atashinda urais, Dk. John Magufuli, kwa kuwatumikia wananchi wetu maana wametuamini na nitaziendeleza miradi ya maendeleo ambayo tunaendelea kuitekeleza jimboni kwetu,” alisema.
Katika jimbo la Bunda Vijijini, mgombea ubunge wa CCM, Boniphace Mwita Getere, alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 12,589 na kumshinda Suleiman Daud wa CHADEMA aliyepata kura 7,547.

No comments:

Post a Comment