SERIKALI imekanusha uvumi ulioenea kuhusu kifo cha Rais
Mstaafu, Benjamin Mkapa na kusema yupo hai, buheri wa afya na yanayosemwa ni
uzushi mtupu.
Aidha, imesema inaendelea kufuatilia chanzo cha uvumi
huo na kwamba itachukua hatua kali dhidi ya atakayebainika kuhusika.
Msenaji Mkuu wa Serikali, Assah Mwambene, alisema hayo
jana, jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa Mkapa ni mzima wa afya na
anaendelea na shughuli zake kama kawaida.
“Rais Mstaafu Mkapa, ni mzima, haumwi hata mafua wala
malaria, tunalaani kitendo hiki cha uzushi na tunatumia nguvu kubwa kuhakikisha
hatua zinachukuliwa kwa aliyeanzisha habari hii,” alisema.
Alisema si jambo zuri kumzushia kiongozi yeyote habari
mbaya kama hizo na kuita kuwa huo ni uchuro, kwa kuwa zilipoanza kusambaa Rais
huyo Mstaafu alikuwa visiwani Zanzibar kikazi.
Alisisitiza kuwa serikali inawataka wananchi kuacha
mara moja kusambaza ujumbe huo unaoenea kwa kasi, ambao si mzuri na
unalishushia hadhi taifa.
Mwambene alisema, Mkapa amekuwa kiungo muhimu kuhusu
amani na mustakabali wa taifa hususani kipindi hiki tangu zilipoanza kampeni za
uchaguzi mkuu.
Kuhusu watu wanaoanzisha habari za uzushi kupitia
mitandao ya kijamii, alisema serikali imekusudia kuongeza kasi ya kuwakamata
watu hao na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment