VIONGOZI wa dini wametakiwa
kukemea watu ambao wanataka kuendeleza migogoro ya kisiasa kwa kuhamasisha
vijana kufanya maandamano ambayo ni kiashiria cha uvunjifu wa amani.
Imeelezwa kuwa vijana wengi
wanakubali kurubuniwa kutokana na kutopenda kujishughulisha, hivyo kulaghaiwa
kwa maslahi ya watu fulani.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Sadiki aliyasema hayo jana, kwenye mkutano wa kuishukuru Kamati ya
Amani ya Viongozi wa Dini mkoani hapa, kwa kuliombea Taifa kufanya uchaguzi
ulio huru na wa amani.
Alisema kuna watu ambao
wanataka kuendeleza migogoro ya kisiasa mara baada ya uchaguzi, badala ya
kuwaza ni namna gani washirikiane na viongozi wateule kwa ajili ya kuleta
maendeleo ya nchi.
Sadiki alisema inapotokea
mtu anachukua majukumu ya tume ya kumtangaza mshindi, ni usaliti na ukiukwaji
wa sheria ambao hauwatakii wananchi heri.
“Watu hao hao ndio ambao
wamekuwa wakisambaza ujumbe kwa wananchi, hasa vijana wakiwataka kuandamana
huku familia zao zikiwa nje ya nchi.
“Vijana wamekuwa wakitumika
na baadhi ya wanasiasa kwa sababu hawataki kufanyakazi, wanataka kupata maisha
kiraisi ndiyo maana baadhi ya watu hutumia fursa hiyo kuwarubuni,”alisema.
Aidha, alitoa wito kwa
vijana kupenda kufanya kazi, hasa mwaka ujao ambao kauli mbiu yake ni ‘Hapa
kazi tu’ ili kuepuka kurubuniwa au kutumika na wanasiasa wenye nia ovu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema
kampeni na shughuli za uchaguzi zimeisha kwa amani na salama tofauti na
ilivyokuwa inategemewa na wengi.
Alisema hayo yote ni
kutokana na maombi yao pamoja na bidiii za mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na
kamati yake ya ulinzi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu amani.
Alisema kama kuna mgombea
yeyote ambaye hakubaliani na matokeo, anapaswa kufuata utaratibu na sheria za
nchi kwakuzingatia katiba inavyosema.
Alhad Salum alisema
wagombea wote walioshinda au kushindwa wanatakiwa kuheshimu damu za wananachi
wasije kutaka kuzitumia kwa maslahi yao ya kutaka kufika wanapotaka.
“Mimi niwaombe waliokuwa
washindani wote, iwe washindi au washindwa, kujiepusha na mambo ambayo yanaweza
kusababisha umwagikaji wa damu za wananchi.
“Kila mmoja anatakiwa
kufahamu kuwa katika kushindana, kuna kushinda na kushindwa, hivyo wakubaliane
na matokeo kwa sababu tume ilikuwa huru,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi
kuendelea kubaki kama Watanzania kwa kuheshimiana bila kuona kuwa huyu ni
mshindi au mshindwa.
No comments:
Post a Comment