Tuesday 12 January 2016

SAMIA: TUMEDHAMIRIA KUJENGA NGUVUKAZI YA VIJANA





MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuijenga nguvukazi ya vijana kupitia kauli mbiu yake ya  ‘Hapa ni Kazi Tu’ kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini.
Samia, ameelezea dhamira hiyo ya serikali katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kulea na Kukuza Wajasiriamali Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhmisho ya kutimiza miaka  52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kilichoko katika Chuo cha Ufundi cha Karume, Mbweni, Zanzibar.
Alisema madhumuni ya kauli mbiu hiyo ni yale yale yaliyoasisiwa na Mapinduzi ya Zanzibar ya kwamba, maendeleo ya nchi huletwa na wananchi wenyewe.
"Tunapozungumzia Mapinduzi ya Zanzibar, lazima tuunganishe na falsafa ya mzee wetu Abeid Aman Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
“Falsafa yake ya kuleta maendeleo Zanzibar na kuifanya ijitegemee, ililenga kumfanya kila mtu awe na taaluma, uweledi na uadilifu kwa kazi anayoifanya, iwe mkulima au mfanyakazi ofisini.
"Lengo lake kubwa lilikuwa ni kujenga nguvukazi inayoweza kuleta maendeleo nchini na hatimaye kujitegemea. Katika enzi hizi tulizonazo, falsafa hiyo inatiliwa mkazo na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ya Dk. John Magufuli,”alisema.
Alisisitiza kuwa kazi ya serikali zote mbili ni kutoa fursa za elimu ili kupata taaluma na ujuzi, pamoja na kuweka miundombinu sahihi ya fursa za masoko.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Ali Abdallah, kituo hicho kimegharimu zaidi ya sh. milioni 300, kwa ajili ya ukarabati, ununuzi wa mashine na kompyuta pamoja na ufungaji wa mashine hizo.
Alisema wazo la uanzishwaji wa kituo hicho limetokana na tathmini iliyofanywa na Dk. Raggive Aggarwal kutoka India, kwa kushirikiana na wataalamu wa SMZ na kubaini kuwa Zanzibar ina fursa nyingi katika kukuza uchumi wake na kuondoa kero zilizopo, hasa ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alisema serikali imeshajipanga kujenga vituo kama hivyo katika kila mkoa wa Zanzibar, vitatu Unguja na viwili kwa Pemba, jambo ambalo limemfanya makamu wa rais kutoa wito wa kuvitunza vituo hivyo ili viwe endelevu na wahitimu wake nao wafuatiliwe kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wao.
Kituo hicho kimekusudia kuangalia maeneo ya kukuza ubunifu wa kuongeza thamani kwa mazao ya kilimo (Agribusiness), ili baadaye kuleta haja ya kuwepo kwa viwanda vidogo vidogo na vya kati, kitatoa elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na elimu ya biashara ya utalii.

No comments:

Post a Comment