Monday, 15 February 2016

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUFANYA TAFITI


Waziri waNishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wawekezaji katika sekta za Nishati na Madini kufanya utafiti wa kutosha katika maeneo husika kabla ya kuendelea na miradi yao.

Prof. Muhongo ameyasema hayo katika mkutano baina yake na wawakilishi kutoka Kampuni ya Lake Holdings ukiwa ni moja kati ya mikutano kadhaa inayoendelea wiki nzima baina ya Wizara na wawekezaji wa sekta hizo.

Kampuni hiyo iliyosajiliwa mwaka 2012, ina mpango ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme chenye uwezo wa Megawati 300 hadi Megawati 450 Wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, ambao ni mkubwa zaidi ukilinganishwa na mradi wa awali wa Kampuni hiyo katika Kata ya Kiwira, Wilayani Rungwe, Mkoani Mbeya, ambao ulilenga Megawati 200 za umeme.

Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa mradi huo, Profesa Runyoro, alieleza kuwa changamoto kuu waliyoipata katika kutekeleza mradi huo ni upatikanaji wa makaa ya mawe, ambayo yanahitajika kwa kiasi kikubwa (tani milioni moja), ili kuwezesha mradi huo, na kuongeza kuwa, maeneo mengi yameshachimbwa na watu wengine.

Akizungumzia suala hilo, Profesa Muhongo aliwataka wawekezaji waache ubahili na badala yake waende wenyewe katika maeneo hayo ili kujua kiasi cha makaa ya mawe yanayopatikana kwani mradi huo ni mkubwa na utahitaji uwekezaji wa kiasi kikubwa na hivyo kuwataka kufanya ‘Geographical Mapping’ na kisha kutoa majibu baada ya mwezi mmoja.

Aidha, alilitaka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufanya kazi kwa karibu na Kampuni hiyo ya Lake Holdings ili waweze kuafikiana juu ya swala hilo, ili wawekezaji hao waweze kupata maeneo ya kuchimbia makaa ya mawe.

Alimalizia mkutano huo kwa kuwataka wawekezaji kutochukua maeneo na kuyaacha na hivyo kupoteza muda wa Watanzania, badala yake aliwataka kuyafanyia kazi ili Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hiyo.

No comments:

Post a Comment