SERIKALI imetangaza bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo inakusudia kutumia sh. trilioni 29. 54.
Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo imelenga kupunguza na kudhibiti matumizi bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa,
hivyo kuhakikisha uwepo wa ufanisi katika matumizi ya serikali.
Akisoma hotuba ya bajeti ya serikali bungeni jana, Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alisema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 2.5, zitatumika kwa ajili ya uanzishwaji wa mahakama ya rushwa na ufisadi.
Dk. Mpango alisema serikali pia imetenga sh. bilioni 72.3, kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU.
Waziri huyo alisema kati ya fedha hizo, sh. trilioni 17.72 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati matumizi ya maendeleo yatakuwa sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote, ambapo sh. trilioni 8.70 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 3.12 ni fedha kutoka nje.
Aidha, Waziri Mpango alisema serikali imetenga sh. bilioni 44.7, kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake ya masingi ya kukagua na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, serikali imefanya marekebisho ya viwango maalumu vya kodi vya bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei wa asilimia tano.
USHURU WA VINYWAJI
Kuhusu ushuru wa vinywaji baridi, Waziri Mpango alisema katika bajeti hiyo, umeongezeka kutoka sh. 55 kwa lita hadi sh. 58, wakati ushuru wa maji ya matunda yaliyotengenezwa nchini kutoka sh. 10 kwa lita hadi 11.
Alisema ushuru wa maji ya matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, umeongezwa kutoka sh.200 hadi 210.
Waziri Mpango alisema ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, mfano kibuku nao umeongezwa kutoka sh. 409 hadi 430 kwa lita.
Aidha, alisema ushuru wa bia zisizo na kilevi, ikijumuishwa na vinywaji vya kuongeza nguvu, umeongezwa kutoka sh. 508 kwa lita hadi sh. 534.
Alisema ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, umeongezeka kutoka sh. 192 kwa lita hadi sh. 202.
Kwa upande wa vinywaji vikali, alisema ushuru umeongezeka kutoka sh. 3,157 kwa lita hadi sh. 3,315.
Bajeti hiyo imepanga kuongeza ushuru kwa sigara zisizo na kichungi kwa asilimia 75, kutoka sh. 11,289 hadi 11,854, kwa kila sigara elfu moja.
KIINUA MGONGO CHA WABUNGE NA MISHAHARA
Waziri alisema katika bajeti hiyo, serikali inakusudia kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano, ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi.
Aidha, itapunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato yanayotokana na ajira kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9. Hatua hii inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi, hatua kwa hatua hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja.
KILIMO
Waziri Mpango, amependekeza kupunguzwa au kuondolewa kwa ushuru na kodi mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zisizokuwa na tija.
Alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini, itaendelea kutoa mikopo ya riba nafuu na masharti yanayozingatia hali halisi ya sekta ya kilimo, ili kusaidia kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo duni kwenda kilimo cha kibiashara.
Waziri alisema katika mwaka fedha 2016/2017, benki hiyo itaendelea kutangaza na kupanua huduma zake kwa wananchi mikoani.
KUBANA MATUMIZI
Kuhusu huduma, alisema serikali imependekeza kuchukua hatua za kupunguza na kudhibiti bila kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa ili kuhakikisha uwepo wa ufanisi kwenye matumizi yake.
Dk. Mipango alisema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha mikutano yote, ikiwa ni pamoja na mikutano ya bodi, mafunzo na semina, inatumia kumbi za serikali na taasisi za umma.
Hatua nyingine ni kutoa kipaumbele kwa taasisi za umma katika kutoa huduma kwa serikali kama vile bima, usafirishaji wa barua, mizigo na vifurushi, matangazo na usafiri, kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Pia, inakusudia kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa watumishi ili kuepuka malipo yasiyostahili, hivyo serikali itaendelea kufanya sensa ya watumishi wote, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasiostahili, kuendelea kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei.
Aidha, kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari, ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi, kupunguza na kuondoa matumizi yasiyo na tija katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maadhimisho na sherehe za kitaifa, matamasha, machapisho na safari za ndani na nje ya nchi zisizo na tija.
Alisema hatua nyingine ni kuhimiza nakala laini za machapisho mbalimbali, hususani yanayozidi kurasa 50, ili kupunguza gharama za uchapishaji, kutunza mazingira na kudhibiti matumizi ya taasisi na mashirika ya umma yasiyowiana na majukumu yao ya msingi na yasiyo na tija.
MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Waziri wa Dk. Mpango, alisema serikali imetenga sh. bilioni 2.5, katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuwezesha uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi.
Pia, imetenga sh. bilioni 72.3, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kuiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Alisema katika bajeti hiyo, zimetengwa sh. bilioni 44.7 kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukagua na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
KUONGEZA MAKUSANYO
Alisema serikali imependekeza kukusanya sh. trilioni 18.46, kutoka mapato ya ndani, ikizijumuisha halmashauri, ambayo ni sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote.
Waziri alisema kati ya mapato hayo, kodi ni sh. trilioni 15.11, sawa na asilimia 13.8 ya Pato la Taifa.
Kwa mujibu wa Dk. Mipango, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni sh. trilioni 2.69 na sh. bilioni 665.4 kwa mtiririko huo.
Alisema makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazokusanya maduhuli, wana uwezo wa kukusanya kiasi hicho cha mapato.
Dk. Mpango alisema serikali itasimamia kwa karibu na kuziba mianya yote ya uvujaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuhakikisha malengo ya ukusanyaji yanafikiwa.
MATUMIZI YA EFD
Kwa mujibu wa waziri huyo, bajeti hiyo imependekeza kuongezwa kwa msukumo katika matumizi ya mashine za malipo za kielektroniki (EFD), ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anatoa risiti, ambapo pia aliwataka wananchi kudai risiti kwenye kila bidhaa na huduma wanayoilipia.
Alisema kufanya hivyo kutaimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ili kutekeleza bajeti kama ilivyopangwa.
Dk. Mpango alisema katika kutimiza azma hiyo, serikali imeunda kikosi maalumu cha kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha wale wote wanaokiuka utaratibu huo wanachukuliwa hatua stahili za kisheria.
“Natoa rai kwa viongozi wote, hususan mawaziri, wabunge, madiwani na viongozi wa dini, kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi wetu kwa kuhakikisha tunadai risiti za EFD pale tunaponunua bidhaa au huduma.
"Aidha, wote mnaombwa kuhamasisha wananchi kudai risiti za EFD. Kila asiyetoa risiti na asiyedai risiti, ajue anatenda kosa na anasaliti jitihada zetu za kuijenga Tanzania mpya,”alisema.
Pia, alisema vituo vyote vya kuuzia mafuta ya petroli vimeagizwa kukamilisha ufungaji wa mashine za EFD, kwenye pampu za kuuzia mafuta hayo ifikapo Oktoba mosi, mwaka huu, ili kuhakisha kuwa serikali inakusanya kodi stahiki.
Alisema serikali itafanya ukaguzi kwenye vituo vyote vya mauzo ya mafuta nchini na kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi agizo hilo.
Dk. Mpango alisema katika kudhibiti misamaha ya kodi inayotolewa kwa wafanyabiashara, watumishi wa umma, mashirika ya dini na taasisi zisizo za kiserikali, kuanzia mwaka ujao wa fedha watalazimika kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazoagiza.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, kodi hiyo itarejeshwa kwa wanufaika baada ya ukaguzi kufanyika na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Pia, serikali itawataka wanufaika kuwasilisha maombi yao katika wizara hiyo kabla ya kuagiza bidhaa husika ili kupata kibali cha uagizwaji wa bidhaa hizo.
Dk. Mpango aliwaagiza maofisa masuuli wote kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato unaofanywa na serikali kuu, mamlaka za serikali za mitaa na mashirika na taasisi za umma ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato.
Aidha, kodi na tozo hizo zitakazokusanywa, zipelekwe benki ndani ya saa 24.
Hata hivyo, kuanzia mwaka ujao wa fedha, utaratibu wa kubakiza sehemu ya makusanyo, yaani mfumo wa ‘retention’, umefutwa.
“Taasisi zote zilizokuwa zikitumia mfumo huo zitalazimika kuwasilisha mapato yote kwenye mfuko mkuu wa serikali. Utoaji wa fedha kutoka Hazina kwenda kwenye taasisi hizo, utazingatia utaratibu wa kawaida kulingana na bajeti iliyoidhinishwa,”alisema
Maofisa masuuli wameelekezwa kuzingatia agizo la serikali la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo yaliyoainishwa, ikiwa ni pamoja na safari za nje ya nchi, mafunzo nje ya nchi, posho za vikao, warsha na makongamano, sherehe na maadhimisho ya kitaifa, ununuzi wa samani.
Pia, waajiri wanatakiwa kuwasilisha kodi ya mapato ya wafanyakazi pamoja na michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati.
“Kwa wale wenye malimbikizo ya PAYE na michango, wanaagizwa kuwasilisha malipo hayo kabla ya Desemba 31, mwaka huu, vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao. Maofisa masuuli, wakuu wa taasisi, mashirika na kampuni binafsi wanaagizwa kusimamia utekelezaji wa agizo hili,”alisema.
Hata hivyo, maofisa hao wametakiwa kutumia mfumo wa nakala laini katika kusambaza nyaraka mbalimbali za serikali zinazozidi kurasa 50, isipokuwa kwa mafungu yanayotakiwa kusambaza nakala ngumu kutokana na matakwa ya kikanuni/kisheria.
Alisema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi makubwa ya gharama za kuchapisha na kudurufu nyaraka hizo na kulinda mazingira. Pia mwaka wa fedha 2016/17, madai yote yanayohusu huduma za umeme, maji na simu yatalipwa moja kwa moja na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutumia bajeti za mafungu husika.
Pia, wameagizwa kulipa kwa wakati ankara za huduma za umeme, maji na simu ili kuepuka malimbikizo ya madai mapya na kufanya ununuzi kwa kutumia Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa IFMS.
Aidha, wazabuni na watoa huduma wametakiwa kuhakikisha wanapatiwa Hati za Ununuzi - LPOs zitokanazo na mfumo wa IFMS, hivyo, kuanzia mwaka 2016/17 hati hizo zitakazotolewa nje ya utaratibu huo hazitatambuliwa kama hati halali za ununuzi.
No comments:
Post a Comment