Friday 10 June 2016

DK SHEIN AMPASHA MAALIM SEIF, ASEMA YEYE NDIYE DIKTETA KWA KUTORUHUSU DEMOKRASIA CUF


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema yeye sio dikteta kwani hajawahi kumfukuza kiongozi yeyote wa kisiasa ndani ya Chama kwa ajili ya kulinda maslahi yake binafsi.

Dk. Shein alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na mabalozi, wenyeviti, makatibu wa matawi na wazee wa CCM, kwenye ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Bububu mjini Unguja.

“Mimi sio dikteta kwani sijaingia madarakani kwa ubabe na mabavu.
Kilichoniweka madarakani ni nguvu ya umma, kupitia uchaguzi wa kidemokrasia na kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 91.

"Sasa huyo anayenitangaza mimi eti ni dikteta, anajua maana ya neno hilo au analitamka ili kuwaridhisha wafuasi wake? Akae akijua kwamba, hawezi kunichafua kwa njia hiyo, kwani kinga yangu ni Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, niliyoapa kuilinda na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliwataka wananchi kupuuza kauli na misimamo ya wapinzani, hasa Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kwani hoja zao hazina nia ya kuwaunganisha Wazanzibar, bali zimelenga kuwatenganisha.

Alisema madai ya Maalim Seif kwamba yeye ni dikteta, ni siasa zilizopitwa na wakati na zinapingana na dhamira ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Dk. Shein alisema aliteuliwa na CCM kugombea urais wa Zanzibar na kwamba, hakutumia nguvu ama ushawishi wowote na aliwekwa madarakani na wananchi kupitia uchaguzi wa marudio uliofanyika Aprili, mwaka huu.

Alisema wakati wa uteuzi wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, hakuwazuia wanachama wengine wenye sifa na uwezo kujitokeza kuwania nafasi hiyo, kama ilivyo kwa vyama vya upinzani, kikiwemo CUF.

Rais huyo wa Zanzibar alisema kimsingi sifa ya udikteta anayo Maalim Seif kwani ndiye amekuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais kupitia CUF, tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na amekuwa akiwatimua viongozi wenzake waliotaka kufanya hivyo.

Dk. Shein alisema katika uhai wake wa kisiasa ndani ya CUF, Maalim Seif amewahi kuwatimua viongozi wenzake kadhaa, akiwemo Hamad Rashid Mohamed, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Chama cha ADC.

Alisema kazi iliyoko mbele ya CCM kwa sasa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020, kwa vitendo ili wananchi waweze kupata huduma bora za kijamii na sio kuendesha malumbano ya kuichafua Zanzibar kisiasa.

Aliwataka wafuasi wa CCM waliofanyiwa vitendo vya hujuma kisiwani Pemba, kutolipiza kisasi na kumwachia Mwenyezi Mungu kwa vile mambo hayo yapo ndani ya uwezo wake.

Kuhusu makosa ya jinai waliyofanyiwa wafuasi hao, Dk. Shein alisema suala hilo linapaswa kuachwa mikononi mwa serikali kupitia jeshi la polisi na mahakama.

Akizungumzia utekelezaji wa ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, kuhusu sekta za afya, elimu, umeme na miundombinu ya barabara, alisema zinaendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Dk. Shein aliwatoa hofu vijana na wananchi kwa kuwaahidi kuwa, tatizo la ajira linaendelea kutafutiwa ufumbuzi, ikiwemo kuanzishwa kwa uvuvi na kilimo cha kisasa na kuimarisha vikundi vya ujasiriamali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema siasa zinazoendeshwa na CCM ni za kupigiwa mfano barani Afrika kwani zimeweza kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa haraka.

Alisema moja ya majukumu ya vyama vya upinzani ni kuishauri serikali iliyopo madarakani mambo mema yatakayoweza kuwasaidia wananchi wa makundi mbalimbali na siyo kutengeneza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii.

No comments:

Post a Comment